Wananchi wa Mwanza wakimsikiliza Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuchunguza na
kuchukua hatua za kurejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Ushirika cha
Nyanza ambazo zilinunuliwa na kutwaliwa na watu binafsi kwa njia za ujanja
ujanja.
Rais Magufuli ametoa agizo
hilo leo tarehe 11 Agosti, 2016 alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mwanza
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.
Dkt. Magufuli amesema Serikali
yake haipo tayari kuwafumbia macho watu wachache waliovifilisi vyama vya
ushirika vya wakulima kwa kujimilikisha mali za ushirika yakiwemo majengo,
viwanda na mashamba na ametaka mali hizo zirudishwe mikononi mwa wananchi.
"Hata kama walichukua
miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo zirudishwe kwa
umma" Amesema Rais Magufuli.
Katika Mkutano huo Rais
Magufuli pia amesema Serikali itafanya oparesheni kubwa ya kuteketeza Makokoro
katika ziwa Victoria ikiwa ni juhudi za kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu
uliosababisha kupungua kwa samaki na kuathiri shughuli za uvuvi na usindikaji
wa minofu ya samaki katika viwanda.
Amebainisha kuwa lengo la
kuchukua hatua hiyo ni kuwezesha samaki wengi kuzaliana ili lengo la Serikali
la kujenga viwanda vya kusindika mazao ikiwemo viwanda vya kusindika minofu ya
samaki lifanikiwe.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo
Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu la
Furahisha linalokatiza barabara ya Uwanja wa Ndege kwenda katikati ya Jiji la
Mwanza.
Daraja hilo litakuwa na urefu
wa meta 46, upana wa meta 3.6 na kimo cha meta 5.5 na ujenzi wake unatarajiwa
kukamilika Mwezi Desemba Mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.455
Akizungumzia ujenzi huo Rais
Magufuli amemtaka Mkandalasi anayejenga Daraja la Furahisha kukamilisha kazi
hiyo Mwezi Desemba Mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, na pia ameagiza Mkandalasi
aliyekuwa akifanya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuendelea na kazi hiyo
ndani ya wiki moja kwa kuwa Serikali imejipanga kumlipa fedha za kazi hiyo.
Pia Dkt. Magufuli ameahidi
kuongeza fedha katika ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Katikati ya Jiji la
Mwanza hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili barabara hiyo ifike hadi uwanjani
badala ya kuishia eneo la Pasiansi.
No comments:
Post a Comment