August 11, 2016

DC KAKONKO AKABIDHI MAGARI MAWILI YA WAGONJWA KITUO CHA AFYA MGAZA


Mkuu wa wilaya ya Kakonko Col. Hosea Maloda Ndagala akikabizi funguo za magari mawili ya kubebea wagonjwa  (hayapo pichani)kwa Mganga Mkuu wa kituo cha afya Mgaza Wilayani Kakonko Dkt Selemani Fadhiri. Wanaoshuhudia wapili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya KakonkoLusubilo Mwakabibi na kushoto ni Diwani wa Kiziguzigu, Renatus Daniel.
 Mkuu wa Wilaya akijaribu moja ya magari hayo.
 Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Col. Hosea Ndagala akiongea na  Madiwani. Watumishi wa Hospital wakati wa hafla ya kukabidhi magari ya wagonjwa katika kituo cha afya Mgaza Wilayani Kakonko
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kakonko akitoa shukrani wakati wa hafla ya kukabidhi magari hayo.
**********
Cosmas Makalla, Kakonko
MKUU wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Maloda Ndagala amekabidhi magari mawili mapya ya kubebea wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser Hard top Ambulance yenye thamani ya dola za kimarekani 18,000 kwa gari moja kwa vituo vya afya viwili Wilayani Kakonko hivi karibuni.

Kanali Hosea Ndagala ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla iliyofanyika katika kituo cha afya Mganza amesisitiza magari hayo kutumika kubebea wagonjwa kama ilivyokusudiwa.

 “Naagiza magari haya ya wagonjwa yatumike vizuri kwa kubebea wagonjwa hasa wanawake wanaokwenda kujifungua na kutunzwa vizuri  ili baada ya miaka mitano ya mkopo yaonekane yakiwa katika hali nzuri. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Aidha ametoa wito kwa watumishi wa afya hususani wahudumu kutumia lugha nzuri wanapowahudumia wagonjwa ili kuondoa malalamiko miongoni mwa wananchi ambao baadhi wamekuwa wakilalamika kuwa hawapati lugha nzuri kutoka kwa wahudumu.

Katika hafla hiyo walihudhuria viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri, makamu Mwenyekiti na waheshimiwa madiwani.

Akitoa wito kwa watumishi Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri Juma Maganga ameeleza kuwa Wilaya ya Kakonko imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa magari ambapo gari lililokuwa likitumika kubebea wagonjwa lilikuwa moja tena chakavu.

“Tunalishukuru shirika la UNICEF kwa msaada mkubwa walioutoa wa magari mawili ya wagonjwa kwani itakuwa ni msaada mkubwa kwa akina mama wanokwenda kujifungua na wale wanaoishi maeneo yenye umbali mrefu”.

Mheshimiwa Juma Maganga ameonya watumishi ambao watayatumia magari hayo vibaya kwa ajili ya shughuli zao binafsi watachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja. Aidha amewaomba waheshimiwa madiwani kutoa taarifa wanapoona magari hayo yanatumika vibaya katika maeneo yao ya Utawala.

Vilevile ameliomba shirika la UNICEF kuendelea kusaidia sekta ya afya katika Wilaya ya Kakonko kwani bado inachangamoto ya vifaa tiba pamoja na miundo mbinu ya hospitali.

Mkurugenzi Mtendaji Lusubilo Joel Mwakabibi ambaye ndiye msimamizi wa magari hayo ya wagonjwa amesisitiza watumishi wa afya kuyatunza magari hayo na kuyatumia kwa mujibu wa maelekezo. Ameahidi kuyafanyia service mara kwa mara na kuyawekea mafuta wakati wote.

Shirika la UNICEF limetoa magari hayo kwa Halmahsuri ya Wilaya ya Kakonko kama mkopo utakaolipwa katika kipindi cha miaka mitano. Magari haya yatakuwa ni ukombozi kwa wakazi wa Wilaya ya Kakonko kwani wataweza kupiga simu na kufuatwa pale walipo ili kukimbizwa katika kituo cha afya kwa lengo la kupata huduma ya afya kwa haraka.

No comments:

Post a Comment