October 06, 2015

TIP TOP CONNECTION YAZINDUA MAGUFULI CUP

Meneja wa kundi la muziki la Tip Top Connection Ally Hamisi Taletate ‘Babu Tale’ (katikati) akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa michuano ya Magufuli Cup, kushoto ni mwakilishi wa vilabu Herry Mzozo na kulia ni Daudi Kanuti Katibu wa kamati ya mashindano DRFA
 ***************
 Na Mwandishi Wetu

Kundi la muziki la TipTop Connection la Manzese jijini Dar es Salaam chini ya Meneja wake Ally Hamis Taletele maarufu kama Babu Tale leo wamezindua mashindano yanayofahamika kwa jina la Magufuli Cup ‘Hapa Kazi Tu’ yenye lengo la kuwaleta vijana karibu na kuwafanya wafanye kazi kama ilivyo kauli mbiu ya mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dr. John Pombe Magufuli.

Tale amesema ameamua kuandaa mashindano hayo ili kuwapa nafasi vijana wanaocheza soka la mtaani kuonekana katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu huku akisisitiza vijana kuwa mbele kwenye kupiga kura kwa kujali amani na utulivu uliopo.

“Nasimamia muziki na nipo karibu na vijana, sababu kubwa ya kuandaa mashindano haya ni kuwafanya vijana wapige kazi. Ajira haiwezi kukuijia nyumbani na hakuna kitu kama hicho duniani kote”, amesema Babu Tale.

“Tumeona hii itakuwa sehemu ya kuwafanya wanasoka ambao wako mitaani waonekane katika msimu huu wa siasa na kampeni ndio maana hata hapa pembeni yangu nipo na watu wa mpira wenye mifano ya watu waliowasaidia kwenye soka”. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Kwa upande wake Daudi Kanuti ambaye ni katibu wa mashindano wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) amevitaja vilabu nane ambavyo vitashiriki michuano hiyo na tarehe rasmi ya kuanza mashindano.

“Jumla ya timu nane zitashiriki michuano hiyo iliyopewa jina la Magufuli Cup ‘Hapa Kazi Tu’. Timu hizo ni Abajalo, Zakhem, Tuamoyo, Burudani FC, FC Kauzu, Goms United, Friends Rangers na Faru Jeuri. Michuano itaanza Octoba 9, ambapo mechi ya ufunguzi itachezwa kati ya Abajalo dhidi ya Zakhem mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Mwl. Nyerere”, Kanuti amesema.

Naye mwakilishi wa vilabu vishiriki vya michuano hiyo Herry Mzozo amewashukuru waandaaji wa mashindano hayo ya Magufuli Cup na kusema hiyo ni fursa kwao kama vilabu na wamefurahi kupata fursa ya kucheza michuano hiyo kwasababu itawafanya vijana waoneshe vipaji vyao lakini pia zawadi zitaleta changamoto kwenye michuano hiyo.

“Sisi kama timu nane ambazo tumeingia kwenye mashindano haya tumeyafurahia sana mashindano. Sisi watu wa mpira tunaangalia mashindano yenye fursa ndani yake ambayo yanafaida moja kwa moja na hayaumizi viongozi wa vilabu kutoa pesa nyingi mfukoni kwa ajili ya gharama za mashindano”, Mzozo amefafanua. 

“Tunapenda watu wawekeze pesa kwa ajili ya mpira na vijana na vitu kama hivi sisi ndio tunavihitaji kwenye soka la leo ili mpira uendelee sio kwa maneno bali kwa vitendo, hii itasaidia soka letu piga hatua mbele. Kwa mfano timu ikiibuka mshindi wa michuano hii inaweza ikafungua biashara na kuisimamia vizuri baadae timu za mtaani zikaacha kuwa tegemezi”.

Mashindano hayo yapotofauti na mashindano mengine yaliyotangulia kwasababu mashindano ya Magufuli Cup kila mechi itakuwa na zawadi. Katika mechi za awali (robo fainali) mshindi atapata shilindi milioni moja na aliyepoteza atapata shisilingi laki tano, hatua ya nusu fainali mshindi atapata shilingi milioni moja na nusu wakati aliyefungwa anapata laki saba.

Hatua ya mshindi wa tatu, mshindi wa mechi hiyo atapata shilingi milioni mbili wakati ayepoteza mchezo huo ataondoka na shilingi milioni moja. Timu zitakazocheza fainali mshindi atapata kitita cha shilingi milioni tano wakati mshindi wa pili atapata shili milioni tatu.

Kwahiyo mshindi wa fainali ya Magupuli Cup ‘Hapa Kazi Tu’ atajinyakulia zaidi ya shilingi milioni kumi za kitanzania

Wakati huohuo waandaaji wa michuano hiyo wamesema watazipatia jezi na mipira timu zote shiriki pamoja na kuzigharamikia nauli za kwenda uwanjani na kurudi kutokana na timu nyingi kusumbuliwa na tatizo la nauli na maandalizi mengine ya mechi.

No comments:

Post a Comment