October 20, 2015

KIIZA MCHEZAJI BORA WA MWEZI SEPTEMBA

Mshambuliaji wa timu ya Simba, Hamisi Kiiza ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Septemba.

Kwa kuibuka mchezaji bora, Kiiza atazawadiwa sh. milioni moja kutoka kwa mdhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom.

Kiiza ambaye ameisadia Simba kufanya vizuri kwenye mwezi huo, ikiwemo kufunga mabao matatu (hat trick) kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar aliwashinda washambuliaji wa timu za Stand United (Elias Maguli) na Yanga (Amisi Tambwe).

Ndani ya mwezi Septemba ambapo zilichezwa raundi tano, Kiiza amefunga jumla ya mabao matano. 

LIGI KUU YA VODACOM KUENDELEA WIKI HII

Ligi kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) inatarajiwa kuendelea kesho Jumatano kwa michezo minne kuchezwa katika viwanja tofauti nchini, huku timu 8 zikisaka kupata pointi tatu muhimu.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Young Africans watawakaribisha Toto Africans, mchezo utakaonza majira ya saa 10:30 jioni, mjini Shinyanga Stand United watakua wenyeji wa Majimaji katika uwanja wa Kambarage mjini humo.

Tanzania Prisons watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku Wagosi wa Kaya, Coastal Union wakiwakaribisha Kagera Sugar katika uwanja wa Mkwakani jijini Tanga.

Alhamis ligi hiyo itanendelea kwa michezo minne pia kucheza katika viwanja mbalimbali, JKT Ruvu wataikaribisha Mtibwa Sugar uwanaj wa Karume jijini Dar es salaam, Mwadui FC watacheza dhidi ya Mgambo Shooting katika uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga.

Jijini Mbeya, Mbeya City watawakaribisha African Sports katika uwanja wa Sokoine, huku Ndanda FC wakiwa wenyeji wa waoka mikate wa bakhresa Azam FC katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

No comments:

Post a Comment