Mchungaji Christopher Mtikila amefariki hii leo katika ajali baada ya gari alilokuwa akisafiria kuacha njia na kupinduka eneo la Msolwa-Chalinze mkoani Pwani.
Mtiklila alikuwa kiongozi wa
chama cha upinzani Tanzania cha Democratic Party (DP).
Mtikila alizaliwa Ludewa Mkoani Njombe, kusini mwa
Tanzania, mwaka 1950.
Pamoja na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa kanisa
la Kipentekoste la Full Salvation Church.
Mchungaji Mtikila amekuwa pia alijihusisha na harakati za
haki za binadamu kwa kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo
kiitwacho Liberty Desk.
Mwanzoni mwa miaka ya 90, mchungaji Mtikila
alijipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa
wa kuongea, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano kati ya Tanganyika
na Zanzibar,
madai yake kuhusu uhujumu wa uchumi unaofanywa na wahindi (ambao anawaita
Magabacholi), na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika
mahakama za Tanzania.
Kwa muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza
kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kutambua Zanzibar.
Alikuwa akisisitiza kuwa chama chake ni cha
Tanganyika na sio Tanzania. Hata hivyo Mtikila alibadili msimamo wake katika
miaka ya karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama toka Zanzibar (kama sheria ya
uchaguzi inavyotaka) na hivyo chama chake kuweza kupata usajili wa kudumu.
Mwaka 1997, Mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM
wakati huo, Horace Kolimba aliitwa na Kamati Kuu ya chama chake mjini Dodoma
kwenda kujibu mashtaka ya ndani ya chama juu ya kauli ambazo alikuwa akizitoa
kwamba “CCM imepoteza mwelekeo”, baadhi ya viongozi wa chama chake
walimchukulia kama msaliti na wengine wakimuona kama mtu aliyethubutu kusema
ukweli bila kumhofia Nyerere. Hata hivyo, Kolimba alifariki hukohuko Dodoma
katika siku ambazo alikuwa akihojiwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipotangaza
uchaguzi mdogo, ndipo Mtikila alikihama chama chake cha DP akajiunga na Chadema
na kuomba ridhaa ya kugombea. Mtikila ni mzaliwa wa Ludewa na alifanya hivyo
kwa sababu chama chake cha DP kilikuwa kimenyimwa usajili.
Uchaguzi ulifanyika Mei 25, 1997 na kumpa ushindi
mgombea wa CCM Profesa Chrispin Haule Che Mponda ambaye alipata kura 20,111
dhidi ya 8,386 za Mtikila. Mgombea wa NCCR ambayo haikuwa imejijenga vilivyo
Ludewa, Barnabas Kidulile, alipata kura 1,271.
Baada ya kushindwa uchaguzi huo, Mtikila alisikika
akihitilafiana na Chadema hadharani huku akitoa shutuma nzitonzito, akafukuzwa
kwenye chama hicho na ndipo akaendelea kuwekeza nguvu kwenye mipango ya
kukamilisha usajili wa chama chake.
Mbio za urais
Mtikila alianza harakati za kugombea urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya DP. Alikuwa kati ya
wagombea 10 katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Katika uchaguzi huo, alipata
asilimia 0.27 ya kura zote, akiwa nyuma ya Jakaya Kikwete wa CCM (asilimia
80.28), Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (asilimia 11.68), Freeman Mbowe wa
Chadema (asilimia 5.88), Augustine Mrema wa TLP (asilimia 0.75) na Dk Sengondo
Mvungi wa NCCR (asilimia 0.49).
Katika Uchaguzi Mkuu unaotaraji kufanyika Oktoba
25 mwaka huu Mtikila kupitia DP, alichukua fomu lakini alishindwa kutimiza
masharti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na jinalake kuondolewa katika orodha ya
wagombea Urais.
Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja
kesi ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi
wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda
Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila
kuomba kibali toka kwa Mkuu wa Wilaya na Polisi.
Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada
ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu
wa CCM, marehemu
Horace Kolimba.
Mwaka 2004 alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa
cha miezi sita kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala.
Mchungaji Christopher Mtikila, mwaka huu mwezi
March alifungua kesi ya kikatiba namba 14 ya mwaka 2015 katika Mahakama Kuu ya
Tanzania kupinga muswada wa mabadiliko ya sheria kwa ajili ya kuitambua rasmi
Mahakama ya Kadhi.
No comments:
Post a Comment