Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju (kushoto) akikaribishwa Wizara ya
Katiba na Sheria kwa shada la maua kutoka kwa mtumishi wa Wizara Bi.
Christina Jenga leo (Jumatano, Januari 7, 2015) jijini Dar es Salaam
huku Katibu Mkuu wa Wizara Bi. Maimuna Tarishi akishuhudia. Bw. Masaju
alifika Wizarani kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Jakaya
Kikwete ili kubadilishana mawazo na viongozi na watumishi wa Wizara.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju akipokewa na watumishi wa Wizara ya
Katiba na Sheria leo (Jumatano, Januari 7, 2015) wakati alipofika
Wizarani hapo kukutana na viongozi na watumishi ili kubadilishana
mawazo.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju (kushoto) akibadilishana mawazo na
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro leo (Jumatano, Januari
7, 2015) wakati alipofika Wizarani kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na
Rais jakaya Kikwete hivi karibuni.
******
Na Mwandishi Wetu
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju amewakumbusha watumishi wa umma
katika sekta ya sheria kufanya kazi kwa ushirikiano na uzalendo ili
kulinda maslahi ya taifa.
Bw.
Masaju, ambaye ameteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais Jakaya
Kikwete kushika wadhifa huo, amefafanua kuwa watumishi wa umma
wanapozingatia uzalendo katika utendaji wao, wanapata nguvu ya kusimama
na kukemea maovu.
Bw.
Masaju ameyasema hayo leo (Jumatano, Januari 7, 2015) jijini Dar es
Salaam alipokuwa akizungumza na viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria
alipokwenda kubadilishana nao mawazo.
“Sisi
kama Wizara kwa ujumla wetu, tunapaswa kuwa mfano wa uzalendo katika
taifa hili ili tunaposimama mbele ya watu, tuwe na nguvu kwa kuwa tupo
safi,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kabla ya uteuzi huo,
alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akizungumza
katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro
alimpongeza Bw. Masaju kwa heshima aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete na
kuahidi kuwa yeye na Wizara itaendelea kumpa ushirikiano wa kutosha
katika kutekeleza majukumu yake.
“Tunakupongeza
kwa heshima kubwa uliyopewa na Mheshimiwa Rais na sisi kama wasimamizi
wa sera, tutaendelea kutoa ushirikiano kwako kama tulivyofanya kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyetangulia,” alisema Waziri Migiro.
Aidha,
Waziri Migiro aliahidi kuongeza ushirikiano katika kuimarisha kada ya
Mawakili wa Serikali pamoja na watumishi wengine ili kuongeza ufanisi
katika utoaji haki.
Bw.
Masaju aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 2 Januari
mwaka huu na kuapishwa tarehe 5 Januari. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Aidha, Bw. Masaju amewahi kuwa
Mshauri wa Sheria wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment