December 13, 2014

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA DODOMA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 13/12/2014

Kama mnavyofahamu kesho tarehe 14/12/2014 ni siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Ni uchaguzi muhimu sana kwani ndiyo uchaguzi unaowaweka madarakani viongozi ambao wapo karibu zaidi na wananchi.

Nataka kuwahakikishia wananchi wote wa mkoa wa Dodoma kwamba  Polisi tumejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola kusimamia usalama siku hiyo. Hivyo wananchi wajitokeze kupiga kura na wala wasiwe na hofu kwani ulinzi utaimarishwa katika vituo vyote vya kupigia kura na maeneo mengine.

Ninatoa wito kwa watu wote kufuata sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi. Kila atakaye maliza kupiga kura arejee nyumbani kwake au kwenye shughuli zake asikae maeneo ya vituo vya kupigia kura. Wanaoruhusiwa kuwepo wakati wote ni wasimamizi wa uchaguzi, wakala wa vyama na askari wa kulinda usalama katika kituo husika.

Tunawataka watu wote wawe watii wa Sheria bila shuruti na atakayekiuka atakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Endapo kuna mtu mwenye malalamiko yoyote kuhusiana na taratibu za Uchaguzi afuate taratibu kama zilivyo ainishwa katika sheria na kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa na siyo kufanya vurugu au kwa kifupi kuvunja sheria.


Imetoliwa na kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment