Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa NHIF Bw. Khamis Mdee wa pili kutoka kulia akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya mfuko huo wakati walipoonyesha tuzo ambazo mfuko huo ulitunukiwa nchini Morocco na Shirikisho la kimataifa la Taasisi za Hifadhi ya Jamii (ISSA) nchini Morocco hivi karibuni. kulia ni Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti, Kutoka kushoto Kaimu Mkurugenzi Tiba na Ushauri wa NHIF, Dk Mkwabi Fikirini na Mkurugenzi wa masoko na Utafiti NHIF,Raphael Mwamoto wakiwa katika mkutano huo uliozungumzia tuzo hizo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa NHIF Bw. Khamis Mdee wa pili pamoja na wakurugenzi wa shirika hilo kulia Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti, Kutoka kushoto Kaimu Mkurugenzi Tiba na Ushauri wa NHIF, Dk Mkwabi Fikirini na Mkurugenzi wa masoko na Utafiti NHIF,Raphael Mwamoto wakionyesha tuzo zilizokabidhiwa kwa mfuko huo kutoka Shirikisho la kimataifa la Taasisi za Hifadhi ya Jamii (ISSA) nchini Morocco hivi karibuni
********
Kwa miaka mingi sasa, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekuwa mwanachama wa mashirikisho mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Shirikisho la kimataifa la Taasisi za Hifadhi ya Jamii (ISSA), Shirikisho la Hifadhi ya Jamii la Nchi za Afrika Mashariki na Kati (ECASSA), na Shirikisho la kimataifa la Uchumi wa Afya (IHEA). Mashirikisho haya husaidia katika kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali, ushauri wa kitaalamu, viwango vya huduma, miongozo ya kiutendaji pamoja na kutumika kama jukwaa kwa wanachama kujenga na kuhamasisha mifumo endelevu katika hifadhi ya jamii. Taasisi hizi za kimataifa vilevile huhusika katika kutoa tuzo kwa Taasisi ambazo zinafanya vizuri katika ubunifu katika maeneo mbalimbali.
Shirikisho la kimataifa la Taasisi za Hifadhi ya Jamii (ISSA) limekuwa na utaratibu wa kushindanisha mifuko ya hifadhi ya jamii duniani kwenye maswala ya ubunifu katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji yakiwemo; kuboresha huduma, utawala bora, matumizi ya teknolojia, ukusanyaji wa michango na matekelezo, uwekezaji, kufikisha huduma kwa wananchi waliyo sehemu ngumu kufikika, uhamasishaji wa Afya na uepushaji wa hatari makazini, pamoja na utekelezaji wa tathmini za uhai wa mifuko. Mashindano haya yalianza tangu mwaka 2008 na hufanyika kila baada ya miaka mitatu.
Tangu kuanzishwa kwa tuzo hizi, Mfuko umekuwa ukishinda tuzo katika maeneo mbalimbali. Mwaka 2008 Mfuko ulishinda tuzo moja ya ubunifu katika kuboresha huduma na mawasiliano kwa wanachama kupitia siku ya wadau (Clients Days).
Mwaka 2011 Mfuko ulishinda tuzo nne katika masuala yafuatayo;
Uboreshaji wa kitita cha mafao yanayotolewa na Mfuko;
Usimamizi wa Mfuko wa Afya ya Jamii: katika kupanua wigo na jitihada za kufikia lengo la afya kwa Watanzania wote;
Utoaji wa mikopo ya vifaa tiba na Uboreshaji wa majengo inayotolewa na Mfuko;
Ugatuzi wa shughuli za Mfuko kwa kufungua ofisi za mikoa kuwasogezea huduma wananchi: Usimamizi bunifu kuongeza ufanisi katika utendaji.
Kwa mara nyingine Mfuko umeshinda tuzo tatu za ubunifu katika sekta ya hifadhi ya Jamii Barani Afrika katika sherehe za kukabidhi tuzo hizo zilizofanyika tarehe 3 Disemba 2014 katika hoteli ya Sheraton mjini Casablanca, Morocco. Tuzo ambazo NHIF ilikabidhiwa ni katika eneo la utoaji wa huduma za matibabu za kibingwa maeneo magumu kufikika, kazi ambayo Mfuko umekuwa ukifanya kwa kushirikiana na wataalamu wa hospitali za rufaa nchini tangu mwaka 2012.
Tuzo nyingine ni katika eneo la TEHAMA katika utayarishaji pamoja na uwasilishaji wa madai ulioanzishwa kwa dhumuni la kupunguza malalamiko ya baadhi ya vituo vya Afya kuchelewa kulipwa madai yao. Kupitia mfumo huu, muda wa ulipaji wa madai hasa katika hospitali kubwa nchini umepungua kwa kiasi kikubwa sana.
Mfumo huu ulianza tangu Januari 2012.
Tuzo ya tatu ni juu ya huduma za matibabu kwa wanachama wastaafu ambayo imeanza tangu mwaka 2011. Fao la wastaafu linalenga kuwapa wananchi ambao walikuwa wanachama wa Mfuko na wenza wao uwezo wa kutibiwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya baada ya kustaafu ajira mpaka mwisho wa maish.
Mfuko utaendelea kufuata miongozo inayotolewa na mashirika ya kimataifa ili kutekeleza shughuli zake kiufanisi na kuhakikisha unatoa huduma bora kwa wanachama wake.
Mfuko vilevile unadhamiria kuendelea kuboresha shughuli zake ili uweze kukidhi viwango vya kimataifa vinavyotolewa na Shirika la viwango la kimataifa (ISO) na hatimaye kuthibitishwa kwa kutimiza viwango hivyo katika kipindi kifupi kijacho.
NHIF Mfuko pia unatarajia kwa kipindi kijacho kuweza kukidhi viwango vilivyowekwa na Shirikisho la kimataifa la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (ISSA) na kupata ithibati ya kukidhi viwango vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment