December 30, 2014

MWAKA UNAKATIKA....TUMESONGA MBELE AMA NYUMA???

 Amani, Heshima na Upendo kwa wana-blog wote.
Kwanza namshukuru MUNGU kwa baraka ya uhai ambayo mimi nawe tunayo mpaka sasa.

Pili nikupe pole kwa harakati za maisha ambazo sote twazipitia kufanikisha yale mema tupendayo. Ni harakati kubwa sana hasa katika kusonga na maisha yetu ya kila siku na pia kuendeleza gurudumu hili la blogs
Nimekuwa nikituma makala, vipindi na kazi zangu kwenu nanyi mmekuwa wakarimu sana kuzipokea. Ushirikiano ambao umenifanya nizidi kujivunia kuwa mmoja wa bloga,Lakini pia, najivunia sana kuwasiliana na kila mmoja wetu hivi sasa ili kuanzisha mjadala wa changamoto zilizo mbele yetu kama JAMII YA WANA-BLOG wenye lengo la kuigusa jamii.

Ningependa tuanze kwa kujiuliza, Je! Tunasonga mbele ama nyuma katika harakati zetu.
 
Nashukuru kwa blogs na tovuti mpya ambazo zinachipuka na kuendeleza nia njema ya kuigusa jamii. Kaka Luta Kamala aliwahi kuandika akijuliza KWANINI TUNA-BLOG? (Bofya hapa) na hata Kaka Chambi Chachage aliuliza kama uwepo wa blogu zetu unakuza ama kufifisha tasnia nzima ya uandishi (Ipitie hapa)

Jibu halisi tunalo mioyoni mwetu kulingana na dhamira tulizonazo. Lakini kwa ujumla, haijalishi ni sababu gani ilikufanya u-blog, mwisho wa safari sote tunajikuta na zao moja ama "mlaji" mmoja ambaye ni JAMII. Bloga awekaye picha anataka kuionesha jamii alichokiona.

Bloga ahabarishaye anataka kuihabarisha jamii. Yule aandikaye Utambuzi anataka jamii ijitambue. Anayeweka kumbukumbu ni sababu anataka jamii ije isome baadaye. Atangazaye biashara anataka jamii ijue palipo na huduma ama biashara husika. Afunzaye mapishi, mitandao, mavazi, mitindo nk, woote wanalenga katika kuielimisha jamii. Kwa maana nyingine sote twaiandikia JAMII.

Na hili ni lengo jema. Lakini swali linarejea kuwa...... Mwaka huu ambao unaomalizika wiki hii unaonekana kuwa hatua gani kwetu?

Logo hapo juu inaonyesha hatua iliyopihgwa katika siku za mwisho za mwaka. Kuanzishwa kwa mtandao wa bloga ambao (ukitumiwa vema) utakuwa chachu ya mabadiliko ya nchi hasa kwa mwaka huu wa uchaguzi.
Ninalowaza ni hili.....

Vipi tunaweza kuweka nguvu na jitihada zetu pamoja kuweza kuitumikia vema na kwa ufasaha jamii yetu???
 
Mafanikio ya bloga mmoja mmoja yanaweza kudhihirisha kuwa TUNAWEZA, lakini tunalostahili kufanya sasa, ni kushirikiana na kuwa makini katika kila jema tutendalo.

Tunapoumaliza mwaka 2014, tuangalie nyuma na kujiuliza, mwaka unakatika....Tumesonga mbele ama nyuma??


Na jibu la swali hili, liwe CHANGAMOTO YETU sote
Baraka kwenu nyote
Heri ya Mwaka Mpya 2015

No comments:

Post a Comment