Umati wa waombolezaji waliohudhuria mazishi ya Bibi Twitikege katika kijiji cha Newland Kiwira Tukuyu wilayani Rungwe.
Na Rashid Mkwinda
Asubuhi ya Disemba 13, 1940 huko katika kijiji cha Katumba wilayani Rungwe, familia ya mzee Mafumu Mlagha ilikuwa katika furaha kwa kumpata mtoto wa kike baada ya kiu ya muda mrefu ya kuwa na mtoto wa kike.
Ilikuwa ni siku ambayo familia hii ilibahatika kuwa na mtoto wa kike waliyempa jina la Twitikege.
Anga la kijiji cha Katumba lenye jua lililowakia mandhari nzuri ya kijani kwenye kijiji kilichoshamiri kilimo cha Migomba na Chai binti wa kike alizaliwa,Ndege wa angani na vipepeo wenye rangi nzuri walioruka kutoka mti mmoja kwenda mti mwingine ilikuwa ni sehemu ya kukamilisha furaha iliyoigubika familia hiyo na kijiji kwa ujumla.
Twitikege aliliona jua kwa mara ya kwanza, familia ya Mzee Mafumu Tabulo Mlagha wa kijiji cha Katumba wilayani Rungwe walijipatia mtoto wa kike waliyempa jina la Twitikege,walijivunia kuwa na uwiano wa watoto wa jinsi mbili, kutokana na kuwa na mtoto wa kiume katika zao la kwanza.
Twitikege kama walivyo watoto wengine wa familia ya kabila la Kinyakyusa alikuzwa na kulelewa katika maadili yanayoshabihi mila na desturi za wenyeji wa maeneo hayo.
Aliishi na kulelewa katika familia ya ukoo wa kichifu, makuzi yake yalikuwa ni sawa na makuzi ya watoto wengine wa kiafrika waishiyo maeneo ya vijijini. Katika zama hizo neema ilitawala kutokana na ardhi ya kaya hizo kustawi kila aina ya chakula na hivyo kumfanya binti Twitikege akue katika neema.
Maeneo mengi ya vijijini kwa zama hizo ardhi`ilikuwa na rutubna tele na hivyo kusheheni mazao ya kila aina na hivyo kufanya uzawa wa wakati huo kuwa na maisha yenye afya bora kutokana na wingi wa chakula kilichopatikana katika maeneo hayo.
Kama ilivyo desturi na mila za kiafrika binti anapofikisha umri wa kuvunja ungo aliangaliwa na kutunzwa kwa kila hali ambapo Twitikege kulingana na makuzi ya kimaadili aliyokulia alipofikisha umri wa miaka 13 mwaka 1953 alichumbiwa na kijana wa kijiji jirani na nyumbani kwao cha Mpuga.
Alikuwa ni Anyitike Gwalamba Mwakwama Mwaibale ambaye kama walivyo vijana wengi wa wakati huo naye alitokea katika familia iliyostaarabika ya wazazi wachamungu walioishi kwa maadili kulingana na mila na desturi za maeneo hayo.
Baada ya kufunga ndoa Twitikege na mumewe Anyitike alichukua dhamana ya kumlea Twitikege wakaishi vyema nao walirithi desturi njema ya wazazi wao,waliishi kwa wema na uadilifu na kuahidi kuishi kwa raha mustarehe katika kipindi chote cha Uhai wao.
Matunda ya ndoa yao yalibarikiwa na hatimaye wakajaaliwa kupata watoto wake kwa waume ambao nao waliwalea na kuwasomesha kama walivyolelewa wao enzi za ujana wao.
Kwa takribani miaka 50 ya ndoa yao walifanikiwa kupata watoto 9 wa kike na kiume,watatu kati yao walitangulia mbele ya haki na kubaki watoto sita.
Kama ilivyokuwa katika malezi yao katika familia zao Twitikege na Mwakwama waliwalea watoto wao kwa maadili na miongozo ya dini bila kusahau mila na desturi za Kinyakyusa ambazo ziliwafanya wamudu kuishi na watu tofauti na kabila tofauti.
Mwaka 2007 ni siku ambayo Bimkubwa huyo Twitikege Mlagha akiwa ametimiza jumla ya miaka 53 ya ndoa yake na mumewe alipata pigo ambalo kamwe hakuweza kulisahau katika maisha yake.
Alimpoteza mumewe Mzee Anyitike Mwakwama Mwaibale ambaye alifariki na kumuachia ukiwa, ingawa alipata faraja kwa uwepo wa wajukuu na vitukuu lukuki waliotokana na watoto wake yeye na mumewe bali pengo la kumpoteza mumewe kamwe halikuweza kuzibwa.
Halikuzibwa pengo la mumewe ndani ya moyo wake, majonzi na fikra za kumpoteza mwenzi wake vilitawala katika fikra zake ingawa alipata faraja ya kutembelewa na wanawe waliokuwa wakiishi maeneo ya mbali na kijijini kwake.
Mara kadhaa niliwasikia wanawe wakihitaji kuomba ruhusa katika kazi zao ya kuja kumuona mama yao na kumpa faraja, ilikuwa ni katika jitihada za kumsahaulisha machungu aliyokuwa nayo ya kumpoteza mwenza wake aliyeishi naye tangu akiwa kijana hadi anazeeka.
Alimkumbuka Anyitike, alikumbuka walivyokuwa vijana, alikumbuka siku ya kwanza kuchumbiwa na Anyitike, alikosa raha akajikuta akilia peke yake na kuongezeka majonzi ya kumkosa mumewe ambaye kadri walivyoishi walizoeana na hata kufikia hatua ya kuwa kama ndugu waliotokana na baba na mama mmoja.
Ni takribani miaka saba tangu aondoke mumewe Anyitike, Twitikege kwa kipindi cha miaka miwili alianza kukumbwa na maradhi ya Uzee na hivyo kushindwa kujihudumia kwa shughuli alizozoea kujihudumia mwenyewe na kujikuta akilazimika kuomba msaada kutoka kwa wajukuu na wanawe walio karibu.
Bimkubwa huyo aliendelea kuugua na kupata matibabu katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya mkoa wa Mbeya na hatimaye mwaka 2014 alichukuliwa na wanawe kuelekea Jijini Dar es salaam kwa ajili ya matibabu.
Ijapokuwa alikuwa katika maradhi bali aliendelea kuwa faraja kwa wanawe kila walipomuona wakiwa pamoja wakizungumza naye hili na lile.
Kila mtoto alipenda kuwa karibu na mama yao ili apate baraka zake hata hivyo kutokana na maradhi aliyokuwa nayo hakumudu kukaa kwa watoto wote kwa wakati wote bali alianza kuzidiwa na homa na kulazimika kulazwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Kila nyumba ya wanaye alipoenda kuishi nyumba hiyo iligubikwa na furaha na Baraka,wajukuu na watoto wakitamani kuwa naye wakati wote wakifurahia uwepo wake katika familia hizo.
Kulazwa kwake kuliacha simanzi kwa wajukuu na watoto wakikumbuka ucheshi wake na matarajio yao ya kumuombea walau arejee katikasiha njema ili arejeshe furaha na Baraka katika nyumba zao kama ilivyokuwa awali.
Haikuwa bahati tena kwa vitukuu, wajukuu na watoto kumuona Bimkubwa huyu akiwa katika hali yake ya awali,Mwenyezi Mungu aliamua kumuita.
Kama ilivyokuwa wakati wa kuzaliwa kwake,tarehe ileile aliyozaliwa ya Disemba 13 ndiyo hiyo hiyo Disemba 13, 2014 akiwa na jumla ya miaka 74 aliaga dunia usiku wa saa 5:00 Jijini Dar es salaam akiacha majonzi makuu na vilio kwa vitukuu, wajukuu na wanawe sita waliopo.
Marehemu aliagwa Jijini Dar es salaam na mwili wake kusafirishwa
Mkoani Mbeya katika kijiji cha Newland kilichopo kata ya Kiwira wilayani Rungwe na kuzikwa Disemba 17,2014 katika makaburi yaliyopo katika mashamba ya familia mkabala na kaburi la mumewe kipenzi.
Apumzike kwa amani!!Aamen!!
No comments:
Post a Comment