Na Mukhsin Mambo
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi Dr. Titus Kamani, amesema ili kwenda na kasi ya maboresho ya wizara hiyo,
inahitajika dhana ya uwajibikaji na uwazi sambamba na kujitolea kwa nguvu zote
katika kufanya kazi.
Waziri Kamani, ameyasema hayo leo
katika mkutano wa kwanza uliowakutanisha wafanyakazi wote wa wizara hiyo,
wakiwemo wastaafu wa mwaka jana katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Temeke
jijini Dar es Salaam.
Amesema kama kuna mtu ambaye ni
kikwazo katika kukwamisha shughuli za wizara, ni bora akawapisha mapema na
kwamba kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa kuifanya kazi kwa uwazi na
akaitaka wizara kufanya kazi na vyombo vya habari kwani ndio njia pekee ya
kuwafanya watanzania wajue wizara inafanya nini.
“Wewe upo ofisini, halafu
unaogopa ogopa vyombo vya habari, kwani unatatizo gani, kuweni wazi mambo yenu
yawe hadharani, watanzania wa Mbeya wayajue, Rufiji mpaka Pemba,
hakuna kufichaficha jambo katika wizara yangu.” Alisistiza Dk Kamani.
Amesema wizara ya maendeleo ya
mifugo na uvuvi ndio moyo wa taifa kwani huwajumuisha watanzania wengi wenye
maisha ya kawaida, lakini amesikitishwa kwa jinsi ambavyo wizara hiyo imekuwa
ikichukuliwa na baadhi ya watu kama ni wizara
ya yenye migogoro na kuleta hasara maeneo mengine.
“N’gombe hawa wamekua wakiingia
kwenye hifadhi, wanapigwa risasi, wanaaribu mashamba ya watu na kuleta njaa kwa
wananchi, ngombe hawa wamekuwa wakiambiwa wanaleta uharibifu wa mazingira kwa
wananchi kwa sababu ya kuhamahama, kama ngombe hawa ungepatikana utaratibu
mzuri wa kuwatunza, kuwahifadhi basi, taifa hili lingeingiza kipato kikubwa
ikiwemo kuuza nyama hadi nje ya nchi, maziwa na kuboresha afya za watanzania”
alisema Dk Kamani.
Dk. Kamani, amesema anafahamu
Wizara yake ina changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yake, ikiwemo
bajeti kuwa ndogo, lakini kwa kutumia taaluma yake pamoja na ushirikiano wa
wafanyakazi wote wa wizara hiyo, anaamini wizara hiyo badala ya kuonekana ni laana
kwa watanzania, itakuwa ni wizara yenye neema kwa watanzania, yenye kueneza
ajira na kipato kwa sababu hakuna jambo lisilowezekana kama kila mmoja atafanya
kazi kwa dhamira moja.
Akizungumzia juu ya ranchi za taifa, waziri Kamani amesema ana nia ya dhati ya
kuona ranchi za
taifa zinafufuka na kutengeneza uchumi imara wa taifa, kuzalisha Ngombe wenye
ubora ambao watatoa mazao ya mifugo yatakayoliingizia taifa hili kipato
kikubwa.
Akizungumzia sekta ya uvuvi,
Waziri Kamani, amesema sekta hiyo ni tabu tupu, amesema leo tunaambiwa kuna
uvuvi haramu, nyavu zisizokidhi viwango, huku wavuvi wakiendelea kuwa masikini,
katika nchi yenye bahari, maziwa na mito
mikubwa kila kona, ameuliza ni kweli wanahitaji bajeti kubwa ya kushughulika na
mambo hayo?.
“Tunahitaji utashi wa kuwasadia
wavuvi wetu, kwa kutoa elimu na kufanya mazungumzo nao ya mara kwa mara,
kuwatembelea maeneo yao ya kazi na kubaini
matatizo yao
kisha kuyafanyia kazi” Alibainisha Dk Kamani.
Kuhusu zao la kuku, Waziri Kamani
amesema sasa hivi kuna tatizo la mayai feki na chanjo feki, alihoji ni kweli
kwamba wafanyakazi wa wizara hiyo haiwajui wahusika au kuna baadhi ya watumishi
ndio miradi yao?
ambapo aliagiza wizara kubaini wanaofanya biashara hiyo feki ambayo inaleta
madhara hasa wakazi wa mjini ambao ni watumiaji wakubwa wa bidhaa hizo.
Awali, kaimu katibu mkuu wa
wizara hiyo Dk Yohana Budeba alipongeza uteuzi wa Dk Kamani, kuingia katika
wizara hiyo kwakuwa ajira yake ya kwanza mwaka 1982 alikuwa chini ya wizara hiyo kama afisa Mifugo wa kata ya Kisongo wilaya ya Arumeru
Mkoani Arusha, hivyo changamoto nyingi anazifahamu, ni mwenzao na anaamini
watashirikiana vyema katika kukabiliana nazo.
No comments:
Post a Comment