December 21, 2013

UZINDUZI WA RIPOTI YA UWEZO

 Msanii Mrisho Mpoto akielezea kupitia mashairi
 Mama Zaida Mgalla akitoa ufafanuzi kwa ripota wa Uwezo TV Bi. Melania Mhagama
 Mgeni Rasmi akionyesha ripoti baada ya kuzindua.

Wakati ambapo asilimia 100 ya watoto wa Darasa la 3 na kuendelea wanapaswa kuweza kusoma na kufanya hesabu za kiwango fulani, matokeo ya Uwezo yanaonyesha kwamba ni wachache tu ndiyo wanaoweza kufanya hivyo.

Katika Darasa la 3, mmoja kati ya watoto wanne anaweza kusoma Kiswahili kwa kiwango sahihi. Shule za binafsi zinafanya vizuri zaidi kidogo kulinganisha na zile za Serikali, ambapo asilimia 61 ya watoto walio na umri chini ya miaka 9 hawawezi kusoma Kiswahili na kufanya Hesabu za Kuzidisha kulinganisha na asilimia 85 ya wenzao walio katika shule za Serikali.

Matokeo haya yalitangazwa na Twaweza, inayosimamia Tafiti ya Uwezo, katika ripoti yake ya tatu ya Tathmini ya Mwaka ya Ujifunzaji. Matokeo haya yamejikita zaidi kwenye tathmini kubwa kabisa ya mwaka kwa ngazi ya kaya inayopima stadi za kusoma na kufanya hesabu za msingi za watoto.

Tathmini ilifanyika nchi nzima mwaka 2012; ikipima watoto 104,568 wenye umri kati ya miaka 7 hadi 16 katika kaya 55,191, katika maeneo (vijiji) 3,752, kwenye wilaya 126 za Tanzania.

Tathmini ya Uwezo inaonyesha kwamba utendaji uko duni nchini kote. Matokeo muhimu yalikuwa:

Stadi ya kusoma Kiswahili
Matokeo bado ni duni na hayajabadilika sana tangu 2011Mtoto 1 tu kati ya 4 (26%) wa Darasa la 3 anaweza kusoma hadithi ya ngazi ya Darasa la 2.

Kwa Darasa la 7, mtoto 1 kati ya 4 (24%) bado hakuweza kusoma hadithi ya ngazi ya Darasa la 2.

Stadi ya kusoma Kiingereza
Matokeo yalikuwa mabaya zaidi kuliko katika Kiswahili

Katika Darasa la 3, 1 tu kati ya watoto 10 (13%) aliweza kusoma hadithi ya ngazi ya Darasa la 2.

Hata katika Darasa la 7, ni watoto 5 kati ya 10 walioweza kusoma hadithi ya ngazi ya Darasa la 2.
Kufanya hesabu
Matokeo yamepanda zaidi kuliko mwaka 2011 lakini bado ni duni
Katika Darasa la 3, zaidi kidogo ya watoto 4 tu kati ya 10 (44%) walioweza kufanya Hesabu za kuzidisha.

Kufika Darasa la 7, mtoto 1 tu kati ya 10 (11%) aliweza kufanya Hesabu ya ngazi ya Darasa la 2.

Matokeo haya yanaonyesha kwamba kundi kubwa kabisa la watoto halipati ujuzi muhimu katika elimu ya msingi. Hata wanapomaliza elimu ya msingi, watoto bado wanashindwa kufanya zoezi la ngazi ya Darasa la 2.

Kuna tofauti kubwa nchini:
Tathmini ya Uwezo inaonyesha jinsi tofauti ya kimatabaka inavyozidi kukua. Watoto katika maeneo ya mijini wanafanya vizuri zaidi kuliko wenzao wa vijijini katika masuala ya kusoma na kuandika.

Watoto wanaotoka kwenye kaya zenye kipato cha juu vilevile walionekana kufanya vema zaidi katika stadi hizi za msingi, sawa sawa na watoto wanaosoma katika shule za binafsi. Ingawa matokeo ya kujifunza kwa ujumla wake ni duni, tofauti hizi zinazozidi kukua zinaonyesha kuwa mfumo wa elimu unawanufaisha zaidi wale wenye hali bora.

Watoto wote, bila kujali umri, darasa au hadhi ya shule walijaribiwa kwa kutumia ngazi ya kusoma na kufanya hesabu ya Darasa la 2. Matokeo muhimu yalikuwa:

Mahali Katika umri wa miaka 9, ni watoto 3 tu kati ya 10 (32%) wa mijini walio na ujuzi huo wa msingi, kulinganisha na mtoto 1 tu kati ya 10 (11%) wa vijijini.

Utajiri Katika umri wa miaka 9, ni watoto 2 tu kati ya 10 (21%) kutoka katika kaya tajiri zaidi walio na ujuzi huo wa msingi, kulinganisha na chini ya mtoto 1 kati ya 10 (6%) kutoka kaya maskini.

Aina ya Shule Katika umri wa miaka 9, ni zaidi kidogo tu ya mtoto 1 kati ya 10 (15%) katika shule za umma aliyefaulu majaribio hayo wakati ambapo ni watoto 4 kati ya 10 (39%) kutoka shule binafsi walioweza kufanya hivyo.

 “Kuna habari kuu mbili katika elimu ya Tanzania leo,” alisema Zaida Mgalla, Mratibu wa Nchi wa Uwezo Tanzania “Kwanza, watoto walio wengi hawajifunzi kitu. Pili, sisi ni jamii ya matabaka mawili – lile lenye utajiri zaidi au la mjini au linaloweza kumudu gharama za shule za binafsi na hivyo watoto wao kufanya vizuri zaidi shuleni kuliko watoto wengine.

Linapokuja suala la elimu, Tanzania si nchi moja.” Tathmini ya Uwezo ya mwaka 2012 iliendeshwa na wananchi waliojitolea 7,560, ambao walisimamiwa na washirika katika wilaya 126 nchini (Wilaya za Mtwara hazikujumuishwa kwa sababu viongozi wa Mkoa hawakuruhusu utafiti kuendeshwa mwaka 2012). Lengo lilikuwa ni kuwashirikisha wananchi katika mchakato wa kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuhakikisha watoto wetu wanajifunza.

Mkuu wa Twaweza, Rakesh Rajani, alisema “Kuinua ubora wa elimu ni jukumu la msingi la Serikali; hata hivyo jukumu hili inatuhusu sote. Hatua zichukuliwe katika ngazi zote, na kila mmoja – kuanzia wazazi hadi watunga sera, kuanzia walimu hadi maofisa wa wilaya – kila mmoja ana mchango wa kipekee katika kuhakikisha watoto wetu wanajifunza.”
Mgeni Rasmi Salum Mjagila, Mkurugenzi, Elimu ya Watu Wazima MOEVT, akikabidhi ripoti kwa mwakilishi wa wanafunzi ambae pia ni ripota wa Uwezo TV, Bi. Fatma Bakari
Rakesh Rajani, John Ulanga, Zaida Mgalla na waalikwa wakifurahia jambo

No comments:

Post a Comment