December 23, 2013

BONANZA LAMTIMUA KOCHA WA YANGA


BRANTS.jpg Leca Kimaro, wa 
Sufiani Mafoto DAR
IKIWA ni siku mbili tu baada ya kufungwa na mahasimu wao Simba mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki wa Nani Mtani Jembe kwenye Uwanja wa Taifa, Klabu ya Yanga SC ya jijini Dar es Salaam, leo imetangaza rasmi kumtema kocha wake mkuu Mholanzi, Ernie Brandts.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Klabu hiyo yaliyopo mtaa wa Jangwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb, leo alisema  kuwa tayari kocha huyo, Ernest Brandts amepewa notisi ya mwezi mmoja kwa mujibu wa taratibu za ajira na baada ya hapo ataondoka.

Aidha Bin Kleb amesema sababu za kumuondoa kocha huyo ni kushuka kwa kiwango cha timu katika siku za hivi karibuni na si vinginevyo kama ambavyo baadhi ya watu wanaweza kutafsiri kuwa huenda ni kutokana na kipigo cha juzi cha mabao 3-1 na ule mchezo wa 3-3 dhidi ya Simba.

“Kweli mwanzoni alipandisha kiwango cha timu yetu, kilipanda sana, lakini baadaye kiwango kikaanza kushuka, tukasema tumpe muda kidogo, lakini tunaona mambo yanazidi kuharibika, hivyo tumeamua kuachana naye,”alisema Bin Kleb
Kuhusu Wajumbe wengine wa benchi la Ufundi, Bin Kleb alisema kwamba taratibu nyingine zinafuata na wakati huo huo klabu inasaka mwalimu mwingine atakayerithi mikoba ya Brandts.

Pia, Bin Kleb amethibitisha ushiriki wa Yanga katika Kombe la Mapinduzi Januari mwakani visiwani Zanzibar na kuongeza kuwa timu inatarajia kufanya ziara ya Ulaya baada ya michuano hiyo.
Pamoja na hayo, Bin Kleb amesema hawezi kuwapongeza watani wao Simba SC kwa kuwafunga 3-1, kwa sababu siku hiyo Yanga ilicheza mpira mbovu na ingeweza kufungwa hata na timu inayoshuka daraja
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga Bin Kleb (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya klabu hiyo leo. Kulia ni Ofisa Habari, Baraka Kizuguto.

No comments:

Post a Comment