May 01, 2013

IDDI SIMBA SASA ASHITAKIWA KWA KUHUJUMU UCHUMI

Mzee Iddi Simba (kulia) akiteta jambo na Wakili Maarufu Said El Maamri mwanzoni mwa kesi hiyo Mahakama ya Kisutu.
 *******
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Iddi Simba aliyekuwa akikabiliwa na mashitaka ya kusababisha hasara katika shirika hilo, amefutiwa mashitaka hayo na kusomewa mapya ya uhujumu uchumi.

Awali Simba na wenzake, walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kusababishia shirika hilo hasara ya Sh bilioni 2.3, kwa kuuza hisa milioni 7.8 za shirika kwa kampuni ya Simon Group, bila kufuata utaratibu wa mchakato wa zabuni.
 
Jana Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta, aliwaachia huru washitakiwa hao, baada ya upande wa mashitaka, kuomba kufuta kesi ya jinai iliyokuwa inawakabili, kabla ya kukamatwa tena na kusomewa mashitaka mapya.
 
Aidha, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena, ameunganishwa katika mashitaka hayo, lakini jana hakufikishwa mahakamani kusomewa mashitaka dhidi yake kwa kuwa bado hajakamatwa. 
Awali Wakili wa Serikali, Osward Tibabyekomya, alidai mahakamani hapo kuwa wakati wanakusanya ushahidi katika kesi hiyo, walibaini kuwa ushahidi huo ni wa mashitaka ya uhujumu uchumi ambayo wanataka kuyaongeza.
 
Hata hivyo, alidai kuwa walibaini wakiongeza mashitaka hayo, wataharibu mwenendo wa kesi hiyo ndio maana wanaiomba Mahakama wafute kesi hiyo na kufungua kesi ya uhujumu uchumi, chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
 
Mbali na Simba ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Tatu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Bodi ya Shirika hilo, Salim Mwaking’inda na Meneja Mkuu wa Shirika hilo, Victor Milanzi.
 
Akiwasomea mashitaka hayo, Wakili Awamu Mbagwa, alidai kuwa katika mashitaka yanayomkabili Simba na Milanzi, kati ya  Septemba 2009 na Januari 2010 Dar es Salaam, walipanga njama kwa nia ya kujihusisha na vitendo vya rushwa katika ununuzi.
 
Alidai kuwa katika siku hizo hizo, Simba na Milanzi, walipokea Sh milioni 320 kutoka kwa Kisema, kama kishawishi cha kuiuzia kampuni hiyo hisa za  Uda.
 
Mbagwa alidai kuwa Simba, Milanzi na Mwaking’inda, wakiwa katika ofisi za Uda, Kurasini, Temeke, Dar es Salaam, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuuza hisa milioni 7.8 za shirika hilo.
 
Mauzo ya hisa hizo zilizokuwa zikimilikiwa na Serikali na Halmashauri ya Jiji la Dar  es Salaam, kwa kampuni ya Simon Group, inadaiwa hayakufuata mchakato wa zabuni jambo ambalo ni kinyume na sheria. 
 
Katika mashitaka mengine, inadaiwa kuwa kati ya Septemba 2009 na Februari 2011, washitakiwa hao walitumia madaraka yao vibaya kwa kuuza hisa kwa Sh bilioni 1.1, bila kuwahusisha wamiliki wa hisa hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
 
Aidha alidai kuwa, washitakiwa hao walisababisha hasara ya Sh bilioni 8.4, na si Sh bilioni 2.3, iliyokuwepo katika mashitaka ya awali kwa shirika hilo.
 
Hasara hiyo inadaiwa kutokana na kuuza hisa hizo kwa Sh bilioni 1.1, wakati kama wangefuata mchakato wa zabuni, wangeuza hisa hizo kwa Sh bilioni 8.4.
 
Hata hivyo, washitakiwa walikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana, baada ya Wakili Alex Mgongolwa, kuomba wadhamini wa awali waendelee kuwadhamini washitakiwa hao.
 
Hakimu Mugeta alikubaliana na ombi hilo kwa kuwa walifutiwa kesi hiyo asubuhi, hivyo wadhamini hao wataendelea kuwadhamini na watahamisha nyaraka za dhamana zilizokuwa katika kesi ya awali. 
 
Wadhamini hao wametakiwa kufika mahakamani Mei 20 na wasipofika, washitakiwa watatakiwa kuwa na wadhamini wengine. Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika. SOURCE: HABARILEO online.

No comments:

Post a Comment