May 03, 2013

AMEND, POLISI KUFANYA MATEMBEZI YA KUUKUMBUSHA UMMA JUU HATARI WAZIPATAZO WATEMBEA KWA MIGUU TANZANIA

Afisa Mpango Mwandamizi Bw. Peter Amos akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu wiki ya nenda kwa usalama barabarani itakayofanyika tarehe 11 Mei, 2013 katika shule ya Sekondari Turiani iliyopo Kinondoni jijini Dar es salaam. 
*******

Na Elphace Marwa - MAELEZO.
SHIRIKA lisilo la kiserikali linalojishughulisha na usalama barabarani AMEND  Organisation kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama barabarani wameandaaa matembezi  mafupi ya kuukumbusha umma kuhusu hatari za barabarani wanazokabiliana nazo watembea kwa miguu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Afisa Mpango Mwandamizi  wa  AMEND Bw. Peter Amos amesema kuwa  kwa kipindi cha mwaka  2012 takribani watu wasiopungua elfu nne walipoteza maisha kwa ajali za barabarani ambapo asilimia 30 kati yao ni watembea kwa miguu.

Bw.Amos amesema kuwa matembezi hayo yatafanyika jumamosi tarehe 11 mwezi mei kuanzia saa tatu asubuhi katika shule ya sekondari ya Turiani wilaya ya Kinondoni.

Aidha Amos amesema matembezi hayo yanalenga kuhamasisha watu kuchukua tahadhari wanapokuwa barabarani ili kulinda usalama wao na watembea kwa miguu.
“Tumejitahidi  kutoa elimu ya usalama barabarani katika shule za msingi na sekondari na kutoa elimu kwa madereva pikipiki kwa lengo la kupunguza vifo na majeruhi wa ajali za barabarani.”

Bw.Amos ameeleza kuwa jumla ya madereva 300 wa bodaboda wamepatiwa mafunzo na wameweza kufaulu vipimo vya udereva  na kupatiwa leseni .

Kwa upande wake Mrakibu wa Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani Bonaventura Nsokolo kutoka trafiki Makao makuu  ametoa wito kwa waandishi wa habari kuelimisha jamii juu ya matumizi bora ya barabara kwani ajali za barabarani zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania wengi wasio na hatia.

Wakati huohuo Afisa Mtendaji Mkuu wa  shirika lisilo la kiserikali la Helmet Vaccine Initiative Tanzania Bw. Alpherio Nchimbi amesema taasisi yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na wadau wengine wana lengo la kupunguza kwa asilimia 50 vifo vinavyotokana  na ajali za barabarani kufikia mwaka 2020.

Wageni rasmi akiwemo  Kamanda Mpinga wa Kikosi cha Usalama barabarani  wanatarajiwa kuzungumza na wananchi siku hiyo ili kuwahamasisha kujilinda na ajali za barabarani na kupunguza vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.

No comments:

Post a Comment