April 10, 2013

Watuhumiwa wa mauaji ya kimbari washitakiwe-Kagame

Na James Gashumba, EANA
Arusha Machi 9, 2013 (EANA) - Rais wa Rwanda Paul Kagame ametoa wito kwa nchi ambazo bado zinawahifadhi watuhumiwa wa mauaji ya kimbari kuwarejesha nchini Rwanda au kuwafungulia mashitaka, linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA).

''Tunashukuru kwamba baadhi ya nchi zimeaanza kufuatilia na kuwatia mbaroni watuhumiwa wa mauaji ya kimbari waliopo nchini mwao, na wengie wamesharejeshwa nchini Rwanda.Hata hivyo hatua hii imekuja ikiwa imechalewa mno wakati nchi hizo zilijua kwa muda mrefu kwamba wanalo jukumu la kukamata watuhumiwa wa mauaji ya kimbari na kuwashitaki, '' Kagame alisema juzi alipokuwa anatoa hotuba yake katika maazimisho ya kumbukumbu ya miaka 19 tangu kutokea mauaji ya kimbari mwaka 1994 nchini Rwanda.

Watu zaidi ya milioni moja waliuawa katika mauaji hayo ya kimbari.
Mtuhumiwa mmoja wa mauaji hayo, Charles Bandora ambaye siku za hivi karibuni alipoteza mapambano yake ya kupinga kurejeshwa Rwanda kutoka Norway, hatimaye alirejeshwa Kigali Machi, mwaka huu.

Alikuwa ni mtuhumiwa wa kwanza kurejeshwa Rwanda kufuatia amri kadhaa za kurejeshwa nchini humo kwa mtuhumiwa mwingine wa mauaji hayo kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Maujai ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) mjini Arusha, Tanzania.

''Bado zipo nchi ambazo zinawahifahadhi watuhumiwa wa mauaji ya kimbari huku wakikataa kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria hata kama upo ushahidi wa kutosha. Nchi hizo lazima zifanye lile linalotarajiwa kuwa ni haki na kuyakubali majukumu yao kupigana na kuadhibu makosa ya mauaji ya kimbari,'' Kagame alisema.

Inaeleweka kwamba kuwafungulia mashitaka au kuwarejesha nchini Rwanda watuhumiwa wa mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita ni wajibu wa nchi yoyote ile na kushindwa kufanya hivyo ni kosa kubwa la kukiuka sheria ya kimataifa.

Licha ya jukumu hilo la kimataifa, mamia ya watuhumiwa wa mauaji ya kimbari bado wanafurahia uhuru wao katika nchi kadhaa za Ulaya,Afrika na nchi za Amerika ya Kaskazini.

Rais Kagame aliahidi kwamba serikali yake itaendelea kuwatumikia walionusurika katika mauaji hayo kwa kuwapatia kila aina ya msaada wanaohitaji.

No comments:

Post a Comment