April 25, 2013

Taswa Queens Yang’ara, Taswa FC hoi

Na Mwandishi wetu
Wakati timu ya netiboli ya waandishi wa habari za michezo nchini, Taswa Queens imeishushia kisago cha mabao 36-2 timu ya kombaini wa walimu wa Wilaya ya Kibiti, wenzao wanaume, Taswa FC imechapwa mabao 2-0 na timu ya kombaini ya Walimu kwa upande wa mpira wa miguu.
 
Huu ni ushindi wa pili kwa Taswa queens tokea kuanzishwa kwake April 6 mwaka huu na kuifunga timu ya Kiliflora queens kutoka mkoani Arusha kwa mabao 28-8 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa TCC, Chang’ombe.
 
Ikicheza kwa uelewano mkubwa, Taswa Queens iliwabana wapinzani wao kila kona na kufunga mabao 18-1 hadi mapumziko. Katika mchezo huo Imani Makongoro kutoka Mwananchi Communications Limited aliyechezea nafasi ya GA alifunga mabao 16 na Amina Mussa wa BTL aliyechezea mafasi ya GS alifunga mabao 20.
 
Wachezaji wengine waliocheza mechi hiyo ni Clensenia Tryphone (Tanzania Daima), Elizabeth Mbassa, Sharifa Mustapha na Johari William wote wa  Business Times Limited (BTL). 
Kwa upande wa soka, mabao yaliyofungwa ndani ya dakika 10  na timu ya kombaini ya walimu, yalidumu muda wote wa mchezo na kuifanya timu hiyo kutoka uwanjani kichwa chini. Mabao ya walimu yalifungwa na Hamidu Mwichande na Juma Kimondoo.
 
Walimu walionyesha uwezo mkubwa katika dakika 25 za mwanzo na kuifanya Taswa FC kutweta katika muda huo, hata hivyo kibao kilibadilika na Taswa FC kutawla muda uliobaki huku ikosa nafasi kadhaa za wazi.
 
Kutokana na kipigo hicho, Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto Omary alisema kuwa wanajipanga kulipiza kisasi kwa kurejea tena kucheza Kibiti. “Tumefungwa kutokana na uchovu sa safari, tulifika saa 9.15 alasiri, tukapata chakula na kwenda moja kwa moja uwanjani, hatukuwa wanyumbulifu, hata hivyo tunaahidi kurejea tena nakulipiza kisasi,” alisema Majuto.
 
Kiongozi wa timu ya walimu, Hamza Malwile, alisema kuwa wamefuraishwa na ujio ya waandishi na kutoa hamasa kubwa ya michezo. Malwile ambaye ni mwenyekiti wa timu, alisema kuwa watajipanga kwa ajili ya mechi ya marudiano.

No comments:

Post a Comment