April 05, 2013

SERIKALI YAPUNGUZA GHARAMA ZA CHANJO ZA MIFUGO

SERIKALI imepunguza gharama za chanjo na dawa za mifugo kutokana na kuanzishwa kwa Taasisi ya Uzalishaji Chanjo za Mifugo Tanzania (TVI) iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Profesa Uswege Minga katika uzinduzi wa maadhimisho wa siku ya Veterinari dunia uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.

Chanjo zinazozalishwa katika taasisi hiyo ni chanjo ya Mdondo (Newcastle disease Vaccine), chanjo ya Kimeta (Anthrax disease Vaccine),chanjo ya Chambavu(Blackquater disease vaccine)  na chanjo ya mtupaji mimba (Brucella Abortus Vaccine).

Alisema kuwa awali Tanzania ilikuwa inaagiza dawa na chanjo hizo kutoka nje ya nchi ambapo ilikuwa inatumia fedha nyingi za kigeni kupata chanjo hizo ambazo hata hivyo zilikuwa hazikidhi mahitaji.

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ilianzisha taasisi hiyo chini ya TVLA ili kuwezesha upatikanaji wa chanjo kwa wakati na kuepuka matatizo yaliyokuwa yanajitokeza kutokana na kuagiza chanjo kutoka nje ya nchi.

Profesa Minga aliongeza kuwa upatikanaji wa chanjo hizo pia umewezesha uchanjaji wa mifugo kwa njia ya kampeni kwa urahisi zaidi kutokana na chanjo hizo kukidhi mahitaji yaliyokusudiwa.

“Kupatikana kwa chanjo hizo pia kumefanikisha kumefanikisha kampeni za uchanjaji katika maeneo yote na kudhibiti ugonjwa uliokusudiwa,kwasababu hiyo magonjwa mengi ya milipuko yamedhibitiwa kuenea hapa nchini”, alisema mwenyekiti huyo.

Maadhimisho ya Veterinari duniani ufanyika kila mwaka mwezi Aprili ambapo wataalam wa mifugo duniani kote hutoa huduma mbalimbali za mifugo ikiwemo chanjo,elimu kwa wafugaji na wadau wengine na maonesho ya mazao ya mifugo.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Chanja ili kuzuia na kulinda” na kilele cha maadhimisho hayo ni Aprili 27, mwaka huu, ambapo wataalam wanahimizwa na kuhamasishwa kutekeleza mikakati na mipango ya kitaifa na kimataifa.

No comments:

Post a Comment