BONANZA
la vyombo mbalimbali vya habari lililopangwa kufanyika Aprili 6 mwaka
huu viwanja vya Leaders Klabu likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA), sasa litafanyika viwanja vya Sigara
(TCC), Chang’ombe pia Dar es Salaam.
Uamuzi wa
kuhamisha bonanza hilo umechukuliwa na sekretarieti ya TASWA kutokana
na maombi ya waandishi wengi wa michezo kwa vile siku hiyo kuna mechi ya
Kombe la Shirikisho la Soka Afrika kati ya timu ya soka ya Azam
na Barrack Young Controllers ya Liberia itakayofanyika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam siku hiyo. Azam
ni timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye michuano ya Afrika kwa ngazi
ya klabu baada ya Simba na Jamhuri ya Pemba kutolewa katika raundi ya
awali.
Tunaamini
kwa bonanza kufanyika Sigara itakuwa rahisi kwa wadau wetu kushiriki
kwenye bonanza na wale wengine watakaohitaji kwenda uwanjani wafanye
hivyo wakitokea Sigara kwa hakuna umbali mrefu na kisha warejee
kujumuika na wenzao mpaka mwisho.
Tunawaomba
radhi kwa mabadiliko hayo, lakini yakiwa na lengo la kujenga na kuwa
pamoja na wenzetu wa Azam kuhakikisha tunashirikiana nao kwa namna
mbalimbali siku hiyo.
Bonanza
hili linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) likiwa na lengo la
kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa,
michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo
mbalimbali vya habari ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Bonanza
hilo ambalo litahusisha wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari
litaambatana na michezo mbalimbali itakayohusisha vyombo vyote
vitakavyoshiriki na pia kutakuwa na burudani ya muziki kutoka katika
moja ya bendi kubwa za muziki wa dansi hapa nchini, ambayo itatangazwa
siku zijazo.
Nawasilisha
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
No comments:
Post a Comment