December 07, 2012

Mama Kikwete apewa tuzo na GAVI Alliance

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo na Taasisi ya Kimataifa ya Gavi Alliance kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii wa kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi vinapungua hapa nchini.
Tuzo hiyo ilitolewa jana usiku katika Hoteli ya Serena na Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi hiyo Dagfinn Hoybraten wakati wa hafla ya utoaji tuzo ilienda sambamba na mkutano wa kimataifa wa siku tatu wa Gavi Alliance unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Akiongea kabla ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mwanamuzi maarufu wa Afrika ya Kusini Yvonne Chakachaka ambaye pia ni Balozi wa heshima wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia watoto Duniani (UNICEF) na mshereheshaji wa shughuli hiyo alisema kuwa hivi sasa wake wa marais wamekuwa wakijitoa kuisaidia jamii hasa katika mambo yahusuyo afya ya mama wajawazito na mtoto.
Mke wa rais wa Zambia Dk. Christine Kaseba Sata naye alipewa tuzo kama aliyopewa Mama Kikwete.
Aidha Wizara za Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Fedha zilipewa tuzo kwa ajili ya kuandaa mkutano huo wa kimataifa wa Umoja wa wadau wa chanjo na Kinga Duniani uliohudhuriwa na wataalamu wa afya, mawaziri wa afya na wake wa marais kutoka barani Afrika.
Mama Kikwete kupitia Taasisi yake ya WAMA amekuwa akitoa vifaa tiba katika Zahanati, vituo vya afya na Hospitali hapa nchini, kutoa elimu kwa jamii na wataalamu wa afya juu ya uzazi salama na afya ya mtoto , wanafanya program ya kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambayo inasaidia mtoto kuzaliwa salama ingawa wazazi wake wanakuwa na maambikizi.
Pia wamekuwa wakiwawezesha wanawake kiuchumi katika miradi mbalimbali jambo ambalo limewafanya waweze kupata kipato cha ziada na hivyo kupunguza makali ya maisha na kuweza kuwatunza watoto wao kwani wanawake wengi wenye kipato cha kutosha wanaweza kuwatunza vizuri watoto wao na kupunguza vifo vinavyoepukika.

No comments:

Post a Comment