Timu ya Taifa (Taifa Stars) imeingia kambini jana jioni (Desemba 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) huku Kocha Kim Poulsen akimjumuisha tena katika kikosi hicho kipa Deogratias Munishi ‘Dida’.
Kocha Poulsen amemjumuisha tena Munishi kwenye kikosi hicho kuziba nafasi ya Mwadini Ally ambaye atakuwa nje ya nchi na timu yake ya Azam inayokwenda kushiriki mashindano maalumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Wachezaji wote wengine walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wamesharipoti kambini hoteli ya Tansoma, na timu imeanza mazoezi leo asubuhi (Desemba 13 mwaka huu) Uwanja wa Karume, na jioni itafanya mazoezi kwenye uwanja huo huo.
Kuanzia kesho jioni (Desemba 14 mwaka huu) itafanya mazoezi Uwanja wa Uwanja wa Taifa wakati mazoezi ya asubuhi yataendelea kuwa Uwanja wa Karume. Wachezaji ambao bado hawajaripoti kambini ni Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira wa kulipwa nchini DRC.
Mechi kati ya Taifa Stars na mabingwa hao wa Afrika itachezwa Desemba 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa. Kocha wa Chipolopolo, Herve Renard ameshataja kikosi chake cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi hiyo.
COASTAL YAENDELEA KUCHACHAFYA UHAI CUP 2012
Coastal Union ya Tanga imeendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya kuwania Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya jana (Desemba 12 mwaka huu) kuifunga Toto Africans mabao 3-1.
Mabao ya Coastal katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Chamazi yalifungwa na Mohamed Miraji dakika ya 44, Abdul Banda (dk. ya 62) na Ramadhan Shame (dk. ya 83). Toto Africans ndiyo iliyoanza kupata bao dakika ya 30 lililofungwa na Severin Constantine.
Coastal Union ilishinda mechi yake ya kwanza mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai.
Nayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon katika mechi ya kundi B iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 12 mwaka huu) Uwanja wa Karume. Miraji Athuman na Ramadhan Mzee ndiyo walioifungia Simba dakika ya 15 na 47 wakati la African Lyon lilifungwa dakika ya 57 na Mbela Kashakala.
Polisi Morogoro iliifunga Azam bao 1-0 kwenye Uwanja wa Karume wakati katika Uwanja wa Azam, JKT Ruvu iliifunga Tanzania Prisons bao 1-0 lililofungwa dakika ya 16 na Jacob Mambia. Yanga na Ruvu Shooting zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Chamazi.
Katika mechi iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 13 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Oljoro JKT imeizamisha Kagera Sugar mabao 3-0. Mabao hayo yamefungwa na Hamis Saleh dakika ya 49 huku Shamir Mohamed akipachika mawili dakika ya 52 na 55.
Michuano hiyo itaendelea kesho (Desemba 14 mwaka huu) kwa michezo kati ya Mtibwa Sugar vs Toto Africans (asubuhi- Karume), Coastal Union vs JKT Ruvu (mchana- Karume), Oljoro JKT vs Yanga (asubuhi- Chamazi), Ruvu Shooting vs Kagera Sugar (mchana- Chamazi), Mgambo Shooting vs Simba (asubuhi- Chamazi) na African Lyon vs Azam (jioni- Chamazi).
No comments:
Post a Comment