Kocha huyo aliyasema hayo mara baada ya Stars, inayodhamniniwa na Bia ya
Kilimanjaro Premium Lager, kumaliza mazoezi katika Uwanja wa Chuo Kikuu
Kyambogo.
“Vijana wamejiandaa vizuri kabisa na wote wako katika hali nzuri ya
kucheza ila tunachoomba ni fair play kutoka kwa muamuzi maana tunacheza na
wenyeji ambao wana watazamaji wengi,” alisema.
Alisema timu zote mbili ni nzuri na iwapo muamuzi atachezesha vizuri
basi utakuwa ni mchuano mkali. “Vijana wana ari na mchezo huu na tukipewa fair
play tutacheza vizuri kama tulivyofanya katika michezo dhidi ya Rwanda,”
alisema Poulsen.
Muamuzi wa mechi ya Cranes na Stars ni Mohamed El Fadil kutoka Sudan
ambaye pia alichezesha mechi ya Stars dhidi ya Rwanda.
Alisema ana furaha kwa kuwa hakuna majeruhi hata mmoja na pia aliwasifu
wachezaji wake kwa kuonyesha umoja na nidahmmu ya hali ya juu. “Hawa wanakaa
kama familia si unawaona walivyo pamoja?” alisema Poulsen na kuongeza kuwa hilo
ni muhimu sana kwa mchezaji.
Naye kocha msaidizi, Sylvester Mash alisema Stars ina nafasi kubwa sana
ya kushinda mechi hii kwa sababu wenyeji wao, The Cranes watakuwa wanacheza kwa
wasiwasi kwa kuwa wako nyumbani .
“Timu yetu iko motivated kabisa na ukizingatia Uganda wako nyumbani, wao
ndio wana tension kubwa zaidi,” alisema na kuongeza kuwa mchezo huu utakuwa wa
kusisimua sana.
Akizungumza kutoka Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium
Lager, George Kavishe alisema Stars ina kila sababu ya kutinga fainali na
kunyanyua kombe kwa mara ya nne.
“Sisi kama wadhamini tunasubiri ushindi maana tuna imani na Stars na
hatua waliyofikia ni nzuri nay a kutia moyo kwa hivyo watanzania wajitokeze kwa
wingi na kuufuatilia mchezo huu kesho,” alisema Kavishe.
Mchezo wa Stars na Cranes utatanguliwa na semi fainali ya kwanza kati ya
Zanzibar na Kenya ambao pia ni mchezo wa kusisimua kwani timu zote mbili
zimeshaonyesha uwezo mkubwa.
Kocha wa Zanzibar Salum Nassor ameshatangaza mara mbili akiwa Zanzibar
na hapa Kampala kuwa iwapo hataondoka na kombe basi atabwaga manyanga.
Fainali na Cecafa Challenge zinatarajiwa kufanyika Jumamosi Disemba 8 na
mechi ya kumpata mshindi wa tatu na nne itachezwa siku hiyo hiyo pia.
No comments:
Post a Comment