Mtafiti kutoka
Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Tanga, Dk. Mercy Chiduo
akiwasilisha utafiti uliofannywa na kikundi cha watafiti wa NIMR nchini,
juu ya uwezo wa dawa ya Ciprofloxacin kutibu ugonjwa wa Kisonono. Taarifa hiyo
ya utafiti huo wa awali ilitolewa mbele ya Waandishi wa habari na Watafiti
mbalimbali jijini Dar es Salaam leo Desemba 2012.
**********
Na Mroki Mroki, FK Blog
UGONJWA
wa zinaa wa Kisonono umekuwa sugu kutibika kwa kutumia dawa ya Ciprofloxacin na
kusababisha wagonjwa kutokukopona.
Kutokufanya
kazi kwa dawa hiyo kutibu ugonjwa wa Kisonono kumegunduliwa na kundi la
watafiti wa Kitanzania kutoka Taaisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)
na Kuongozwa na Mr. John Changalucha, wa NIMR Mwanza na kufanya utafiti juu ya
ufanyaji kazi wa dawa hiyo kwa kutibu kisonono katika wilaya za Tanga, Moshi
mjini, Dar es Salaam.
Akiwasilisha
taarifa ya awali ya utafiti huo uliofanyika kuanzia Oktoba mwaka 2011 na
kumalizika Aprili mwaka huu kwa hizo tatu kabla ya watafiti hao kumalizia
Wilaya ya Mbeya Mjini, Dk. Mercy Chiduo kwa niaba ya Watafiti wenzake amesema
Wilaya ya Moshi mjini ndio tatizo limebainika kuwa kubwa zaidi.
Dk.
Mercy ameeleza kuwa Wilayani Moshi wagonjwa wote waliofanyiwa utafiti
walionesha kutokupona kwa dawa hiyo ya Ciprofloxacin sawa na asilimia 100, huku
Wilaya ya Tanga ulikuwa kwa asilimia 25 na Dar es Salaam ikiwa ni kwa asilimia
71.4.
Aidha
mtafiti huyo anasema uwezo wa dawa hiyo kutibu Kisonono kwa utafiti huo ni sawa
na asilimia 40 hivyo kuwa kinyume na sheria ya Shirika la Afya Duniani ambalo
linagiza kuwa dawa ili iwepo katika orodha ya kutibu magonjwa husika ni lazima
iwe na uwezo wa kutibu kwa asilimia 95.
Watafiti
hao wamependekeza dawa za ceftriaxone, cefixime, azithromycin na spectinomycin
zitumike kwa sasa kutibu ugonjwa wa Kisonono huku Ciprofloxacin ikibaki kutibu magonjwa
mengine isipokuwa Kisonono.
Wagonjwa wapatao 353 walijitokeza katika utafiti huo katika vitengo vya Magonjwa ya
Zinaa kwenye vituo vya afya vya Ngamiani jijini Tanga, Majengo mjini Moshi, na
Zahanati ya IDC Jijini Dar es Salaam.
Kushindwa
kwa dawa hiyo kutibu kunatokana na ugonjwa huo kuwa sugu kufuatia tabia ya wagonjwa wengi kujinunulia dawa bila kupatiwa
vipimo vya daktari na hili linadaiwa kutokana na kuwepo kwa maduka ya dawa
ambayo huwauzia wagonjwa dawa bila kuwa na vyeti vya daktari.
Utafiti
huo wa uwezo wa dawa hiyo kutokutibu unakaribia kuendana na ule uliowahi
kufanyika katika nchi za Israel (61%), Urusi (68%) Kanda ya Magharibi ya WHO (62%-70%),
Afrika Kusini (42%), Japan (24.4%) na China (34.3%), huku Jiji la Mwanza-Tanzania, likionesha dawa hiyo kutokufanya kazi kwa asilimia 71 katika utafiti
uliofanyika mapema.
No comments:
Post a Comment