MUUNGANO wa Vyama vya Waandishi wa
Habari nchini (UTPC) uimeikabidhi Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha
(APC) vifaa vyenye thamani ya Sh. Milioni 35.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa jana Ofisa
Utawala na Fedha wa UTPC Jackosn Uiso katika ofisi za Klabu ya APC jijini hapa
na kushuhudiwa na viongozi na baadhi ya wanachama.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa
hivyo Uiso aliwahimiza viongozi kuhakikisha vinatumika kwa wanachama ikiwa ni
pamoja na kuingizia fedha Klabu.
“UTPC inawahimiza mtumie vifaa hivi kwa
uangalifu, lakini hakikisheni mnaweka utaratibu wa jinsi gani vitawaingizia
fedha za Klabu badala ya kuendelea kuvifungia,” alisema Uiso.
Baadhi ya vifaa vilivyokabidhiwa ni
pamoja na Mashine ya kudurufu, Televisheni ya Inchi 32, Kamera kubwa ya kisasa
kwa ajili ya picha za mnato, mashine ya Projector, Desk Kompyuta na Laptop.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa APC Claud
Gwandu aliwashukuru UTPC kwa kukabidhi vifaa hivyo na kuahidi kwamba vitatumika
kwa uangalifu mkubwa.
“Vifaa hivi ni vya thamani na tunaahidi
kuvitumia kwa uangalifu utakaoleta manufaa kwa Klabu na wanachama wake,”
alisema Gwandu.
Naye Katibu Mkuu wa APC Eliya Mbonea kwa
upande wake aliwashukuru UTPC kwa kufanyia kazi mawazo ya viongozi wa Klabu
nchini waliopendekeza kutumiwa vifaa vinavyolingana na taaluma.
“Mapendekezo ya viongozi wa Klabu
yamefanyiwa kazi, awali tulikuwa tunaletewa kamera ndigo zinazowapa wakati
mgumu waandishi kupiga picha hususani viongozi wa kitaifa wanapokuja au tukio
linapokuwa mbali,” alisema Mbonea na kuongeza:
“Mfano hii Kamera ya picha za mnato
kweli hapa sasa hatuwezi kulalamika tena kwamba hatuna kamera ya kisasa kwani
Kamera hii unaweza kupiga picha ukiwa mahali popote,” alisema.
No comments:
Post a Comment