November 14, 2012

Taifa Stars yainyuka Haranbee Stars 1-0

Mshambuliaji wa timu ya Tiafa Stars, Mbwana Samata akijaribu kumtoka Beki wa Harambee Stars wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Harambee Stares ya Mwanza iliyochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana. Kilimanjaro Stars inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro.


BAO la Aggrey Morris lilitosha kuipa Taifa Stars ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya atika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Morris alifunga bao hilo pekee katika dakika 7 akiunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Amir Maftah.

Kwa matokeo hayo Stars imefanikiwa kulipa kiasi cha kufungwa mabao 2-1 kwenye uwanja huo na Kenya mwaka 2009.

Akizungumza baada ya mechi kumalizika kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen alisema amefurahishwa na ushindi alioupata.

"Taifa Stars ilikuwa haijakaa pamoja kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, hivi sasa ndiyo tumepata nafasi ya kujiandaa kwa muda wa siku mbili na kucheza mechi hii, naamini wachezaji wanastahili pongezi kwa ushindi tulioupata,"alisema Poulsen.

Alisema,"tutatumia muda tulionao kujiandaa, kwani tumeweka kambi hapa Mwanza kwa ajili ya kujiandaa, naamini muda tulionao hivi sasa unatosha kuiandaa timu, siku zote maandalizi ndiyo kitu muhimu."

Naye kocha wa timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars', Henry Michel alisema,"sijafurahishwa na mechi hii, kiwango hakijaniridhisha."

Taifa Stars ilianza mchezo kwa kasi na dakika ya kwanza Ngassa alipiga shuti la mbali lililotoka nje kidogo ya goli, nao Kenya walijibu mapigo kupitia Denis Oliech aliyekosa bao la wazi akiwa yeye na kipa Juma Kaseja.

Stars ilipata bao la kuongoza katika dakika 7 kupitia nahodha wake msaidizi Morris aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Maftah.

Baada ya bao hilo Taifa Stars iliendelea kupeleka mashambulizi katika lengo la Harambee Stars, ambapo mshambuliaji wa  Thomas Ulimwengu wa Taifa Stars alipoteza nafasi mbili za wazi za kufunga katika dakika 13 na 14 akiwa yeye na kipa kwani mashuti yake yalitoka nje.

Vilvile Mrisho Ngasa na Mbwana Samata waligongea pasi na kuwatoka walinzi wa Kenya, lakini kipa wa Kenya, Fredrick Onyango alikuwa makini kuokoa hatari hiyo.

Katika mchezo huo Kelvin Yondani, Samata na Morris walionyeshwa kadi za njano kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya.

Stars ilicheza vizuri katikati ya uwanja, ambapo viungo Abubakari Salum, Frank Domayo na Mwinyi Kazimoto walifanya kazi kubwa ya kutuliza mpira na kugongeana pasi fupi fupi za chini na kupitisha mipira mizuri kwa Ulimwengu, Samata na Ngassa waliokuwa mwiba kwa ngome ya Harambee Stars kutokana na kasi yao.

Kenya wenyewe walitumia zaidi mipira ya juu kuwapitishia Oliech, Ugine Sike na Edwin Wafula waliotumia vizuri urefu wao kucheza mipira ya juu.

Kocha wa Kenya, Michel aliwapumzisha Jerry Santo, Patrick Obaya na Jonas Stima na kuwaingiza Christopher Wekesa, Timbe Ayoub na Antony Akumu.

Naye Kim aliwatoa Kazimoto, Ngasa, Samata, Ulimwengu, Maftah na kuwaingiza Amri Kiemba, Simon Msuva, Christopher Edward, John Bocco na Shaban Nditi.

Mabadiliko hayo hayakuweza kubadilisha mchezo huo kwani washambuliji wa Stars walipoteza nafasi kadhaa za kufunga wakiwa wao na kipa Onyango aliyekuwa kikwazo kikubwa kwao.

Taifa Stars itaendelea na kambi yake jijini Mwanza kujiandaa na mashindano ya Chalenji yatakayoanza Novemba 24, jijini Kampala.

VIKOSI
Taifa  Stars
Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Frank Domayo, Abubakari Salum, Mwinyi Kazimoto, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samata na Mrisho Ngassa.

Harambee Stars
Fredrick Onyango, Brian Mandela, Ugine Asike, Jonas Stima, Edwin Wafula, Jerry Santo, Jerry Opiyo, Patrick Oboya, Patrick Osiako, Denis Oliech na Wisley Keman.
Chanzo:Mwananchi Online

No comments:

Post a Comment