November 29, 2012

HATUJAKATA TAMAA-POULSEN


Kocha wa Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema hajakata tama baada ya kufungwa na Burundi bao 1-0 wakati wa mashindano ya Tusker Cecafa Challenge yanayoendelea Jijini Kampala.

Kocha huyo alisema wakati wa mzazoezi kuwa  vijana wake walijituma sana na kuwasumbua Burundi katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wenye tope zito baada ya mvua kubwa kunyesha Kampala na hivi kuzipa timu zote wakati mgumu.

“Vijana walicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi hivi kuwapa Burundi shida…mabao tuliyokosa ni mengi kwa hivyo hatujakata tamaa…nimeongea na wachezaji na wamenielewa kwa hivyo tunajiandaa vizuri kabla ya kucheza na Somalia Jumamosi kukamilisha hatua ya makundi,” alisema.

Amesema ukiachia Shomari Kapombe na Mwinyi kazimoto waliojeruhiwa wakati wa mechi dhidi ya Burundi, wengine wote wako katika hali nzuri na wanajiandaa kuikabili Somalia.

“Tayari tumeshinda mechi moja dhidi ya Sudan kwa hivyo tukishinda mechi ya Jumamosi tutakuwa katika nafasi nzuri sana ya kuendelea na mashindano haya,” alisema Poulsen.

Mpaka sasa Burundi inaongoza Kundi B kwa pointi Sita, ikifuatiwa na Tanzania na Sudan ambazo zina pointi  tatu na Somalia inashikilia mkia bila pointi yoyote.

Baadhi ya watanzania wanaoishi Kampala wamesema wana imani kubwa sana na timu yao kwani imeonesha uwezo mkubwa sana katika mashindano haya.

Mmoja wa mashabiki aliyesafiri mpaka Kampala kuishangilia Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Ali Shaban alisema kuna matumaini makubwa ya Stars kufika mbali katika mashindano hayo.

“Tumeona mechi yao ya kwanza nay a pili na kwa kweli timu iko vizuri…hatukuwa na bahati ti wa mchezo dhidi ya Burundi lakini timu ilionyesha uwezo mkubwa na hatuwezi kuwalaumu kwa kufungwa kwa penalty,” alisema.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe akizungumza kutoka Dar es Salaam alisema bado kuna matumaini makubwa na watanzania wasife moyo kwani Stars imeshaonyesha uwezo mkubwa na bado kuna nafasi ya kusonga mbele.

“Tunaofuatilia mashindano haya kwenye runinga tumeshuhudia ni jinsi gani vijana wanajituma na ari waliyo nayo ya kushinda,” alisema.

Wakati wa mazoezi, wachezaji wa Stars walipata semina fupi kutoka kwa wawakilishi wa Wash United ambalo ni shirika linalohamasisha unawaji wa mikono.

Shirika hili limeiningia katika makubaliano na shirikisho mbalimbali za mpira duniani ili kuhamasisha wacezaji kueneza ujumbe kuhusu unawaji wa mikono.

No comments:

Post a Comment