April 03, 2012

Ukifayiwa uhalifu Mwanerumango utakiona cha moto!

 Ofisa Mtendaji Kata ya Maneromango, Nicolaus Lemma 
 Mmoja wa wakazi wa Kata ya Maneromango
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Maneromango Sokoni aliyezungumza na mtandao huu


UKIWA wewe ni mkazi wa Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani huenda siku zote utakuwa ukiomba isitokee umeibiwa au kufanyiwa kitendo chochote cha uhalifu kwani utagharamika na kama hauna uwezo kifedha unaweza kumsame mwizi wako bila kupenda.

Hii ni kutokana na utaratibu uliopo eneo hilo ambapo mtu anayeibiwa hulazimika kumgharamia mtuhumiwa pamoja na mgambo fedha za nauli kwenda mjini Kisarawe ili akafunguliwe mashtaka. Mwananchi aliyeibiwa atalazimika kumlipa pia posho mgambo na nauli ya kurudi Maneromango baada ya kumkabidhi mtuhumiwa Polisi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya wakazi wa Maneromango mtu aliyeibiwa au kufanyiwa uhalifu hulazimika kutoa kiasi cha sh. 35,000 fedha ambayo hugharamia nauli ya mtuhumiwa kwenda Kisarawe, nauli ya mgambo anayeambatana na mtuhumiwa kwenda na kurudi pamoja na posho kwa mgambo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi kutoka Maneromango, Rehema Zomboko mkazi wa Kijiji cha Boga Kata ya Maneromango alisema utaratibu huo umewafanya wanakijiji wengi kutotoa taarifa za wizi kwa kile kuogopa gharama za kumsafirisha mtuhumiwa wako.

Akizungumza mkazi mwingine wa Kijiji cha Mengwa, Ramadhan Kingungu alisema utaratibu huo umekuwa kikwazo cha kuambana na vitendo vya kihalifu, kwani wengi wapo radhi kukubali kuibiwa na kumalizana kwa mazungumzo na mtuhumiwa kuliko kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji.

“Katika hali ya kawaida unaweza kuangalia ndugu mwandishi hivi mtu anaweza kukuibia kuku alafu ugharamie sh. 35,000 ili akashtakiwe mjini Kisarawe...? Wengi wameshindwa wanaotoa gharama hizo ni watu wenye uwezo kifedha hapa kijijini,” alisema Kingungu.

Naye Halima Mwinyimkuu wa Kijiji cha Maneromango Kaskazini alisema wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu mara kadhaa (hasa wizi wa kuku) lakini wamekuwa hawachukuliwi hatua zozote kwa wahusika kuhofia gharama za mashtaka.

Aidha akizungumzia utaratibu huo Ofisa Mtendaji Kata ya Maneromango, Nicolaus Lemma alisema ni kweli wananchi hulazimika kuchangia kiasi cha fedha pale wanapokuwa na mtuhumiwa fedha ambazo hutumika nauli kwa mtuhumiwa, mgambo pamoja na mlalamikaji.

“Ni kweli wanalazimika kuchangia lakini si sh. 35,000 kama wanavyosema wao, kiasi cha fedha mara nyingi huweza kufikia sh. 20,000 hivi...hii ni kutokana kwamba hatuna kituo cha polisi katika kata yetu ya Maneromango, lakini juhudi zinafanywa ili tuweze kuwa na kituo,” alisema Lemma.

Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

No comments:

Post a Comment