April 03, 2012

Ripoti ya watalii ipo tayari

Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Nuru Millao akiinua juu ripoti ya watalii waliondoka nchini mwaka 2010 ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa ripoti hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Ibrahim Mussa akipitia kwa umakini kurasa za ripoti hiyo, leo, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu alisema ripoti hii ni muhimu kwa maendeleo ya sekta yetu ya Utalii kwani pamoja na kutupatia taarifa mbalimbali za Utalii lakini pia inatupa taarifa ya changamoto ambazo tunazo katika sekta hii na hivyo kuweza kuzifanyia kazi kwa muda muafaka. “Natoa wito kwa wadau wote wa utalii watumie matokeo ya ripoti hii kuboresha shughuli na huduma zao katika kutangaza utalii na kuandaa mazao (products) ili kuwavutia watalii wengi,” alisema Naibu Katibu Mkuu.
**************

Ndugu wageni waalikwa na waandishi wa habari,

Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ninapenda kuwakaribisha leo katika uzinduzi wa ripoti ya watalii waliondoka nchini mwaka 2010.

Pia napenda kuchukua fursa hii pia kuwapongeza watalaam na wasimamizi kwa kukamilisha na kuchapisha taarifa hii ambayo ni muhimu katika mipango ya maendeleo ya sekta ya utalii hapa nchini. Kama mnavyofahamu sekta ya Utalii imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza pato la taifa na pia fedha za kigeni nchini.

Ripoti hii ya watalii wanaonondoka nchini huandaliwa  kila mwaka ili kujua hali halisi ya sekta ya utalii kwa mwaka husika. Taarifa inayotolewa inasaidia kujua mambo yafuatayo :

·        Wastani wa fedha anazotumia mtalii kwa siku
·        Wastani siku ambazo mtalii kwa kwa wakati wote anapokuwa nchini
·        Masoko /nchi zinazoleta wageni wengi nchini
·        Mapato ya jumla yanayotokana na bishara ya Utalii kwa mwaka husika.
Hivyo basi mtakubaliana na mimi kwamba ripoti hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta yetu ya Utalii kwani pamoja na kutupatia taarifa mbalimbali za Utalii lakini pia inatupa taarifa ya changamoto ambazo tunazo katika sekta hii na hivyo kuweza kuzifanyia kazi kwa muda muafaka.

Natoa wito kwa wadau wote wa utalii watumie matokeo ya ripoti hii kuboresha shughuli na huduma zao katika kutangaza utalii na kuandaa mazao (products) ili kuwavutia watalii wengi.

Lengo kubwa la mkutano huu wa leo ni kuwafahamisha wadau wote wa sekta ya Utalii kuwa ripoti ya watalii waliondoka mwaka 2010 ipo tayari kwa matumizi. Nakala za ripoti hii zitapatikana hapa wizarani, Benki Kuu, Ofisi ya taifa ya Takwimu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment