April 13, 2012

KONGAMANO LA 26 LA KISAYANSI KUFANYIKA JIJINI ARUSHA


Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya NIMR Dk. Mwele Malecela (kulia)  akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu
 Kongamano la Kisayansi litakalofanyika kuanzia  tarehe 16-19 April, 2012 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC mjini Arusha.
Kongamano hilo litatoa fursa kwa wanasayansi, wakufunzi, watoa maamuzi na watunga sera; waandishi wa habari na jamii kwa ujumla; kupata taarifa za matokeo ya tafiti mbalimbali za afya ya binadamu na kubadilishana uzoefu kuhusu ubooreshaji wa afya ya jamii na utafiti wa afya kwa ujumla.


Kauli mbiu ya kongamano hili kwa mwaka huu wa 2012 ni “Mafanikio ya Sekta ya Afya katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia: Kuelekea 2015”.
Kongamano litafunguliwa rasmi tarehe 16 April 2012 – na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DAKTA MOHAMED GHARIB BILLAL.
Kongamano hili la Kisayansi ambalo limekuwa likiandaliwa kuanzia mwaka 1982 na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu–NIMR; litafanya makongamano madogo sita yatakayoendeshwa kwa kuzingatia kaulimbiu ambayo inalenga kutathimini Mafanikio ya Sekta ya Afya katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia: Kuelekea 2015
Makongamano hayo madogo yatajadili masuala mbalimbali yakiwemo
1)   Magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza
2)   Tafiti kuhusu udhibiti wa ugonjwa wa matende na mabusha
3)   Miaka 50 ya uhuru: Mchango wa Utafiti katika sekta ya Afya
4)   Vita dhidi ya Malaria: Nini Kifanyike
5)   Mchango wa utafiti katika kuboresha,  kurekebisha au kutunga sera
6)   Vipaumbele vya Taifa vya Utafiti kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kwa mwaka 2011/2012.


Malengo ya Kongamano
Kongamano hili linalenga kuwashirikisha watafiti, watunga sera na wadau wa afya duniani ili kubadilishana uzoefu katika Nyanja mbalimbali za kisayansi.
Watafiti mbalimbali kutoka katika nchi za Afrika zikiwemo Tanzania, Afrika ya Kusini, Senegal, Marekani na Zambia wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo ambapo mbalimbali zipatazo  zitajadiliwa.

Ni matarajio ya Taasisi kuwa katika kipindi cha siku nne cha kongamano hilo, washiriki wataweza kufikia maazimio kuhusu hatua iliyofikiwa na Tanzania katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya milenia kuelekea mwaka 2015, na pia kuweza kupanga vipaumbele vya utafiti wa ugonjwa wa ukimwi katika mwaka 2011-212.
Vilevile katika harakati za kuhamasha watafiti waliobobea na wale wanaokua katika utafiti; NIMR inatarajia kutoa Tuzo za Kisayansi nne kwa mawaka huu wa 2012 kama ifuatavyo:
1.   Outstanding Scientist of the Year Award 2012 (Tuzo ya Mwana Sayansi Bora wa mwaka) :
Tuzo hii pia inatolewa kwa mara ya kwanza na NIMR ili kutambua kazi zinazofanywa nawatafiti nchini. Inatolewa kwa mtafiti bora nchini ambaye kazi zake za utafiti zimeweza kuleta mabadiliko katika masuala mbalimbali yakiwemo ya uvumbuzi wa teknolojia au mifumo ya utoaji huduma katika sekta ya afya au uvumbuzi ambao umechangia kuundwa au kurekebishwa kwa sera katika sekta ya afya nchini.
2.   Mount Kilimanjaro Scientific Award
Mwanzilishi wa Tuzo hii ni Dakta Leonard Mboera , ambaye ni Mkurugenzi wa TEKNOHAMA-NIMR. Tuzo hii inatolewa kwa mwanasayansi bora, ambaye ni chipukizi aliyewasilisha vyema mada za kiutafiti katika kongamano hili la kisayansi.Tuzo hii inalenga  kuhamasiha wanasayansi chipukizi kushiriki zaidi katika kazi za utafiti.

3.   Dr. Maria Kamm Best Woman Scientist Award
Tuzo hii inatolewa kwa mara ya kwanza mwaka huu na imeanzishwa rasmi na Dakta Mwele Malecela ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR. Lengo la tuzo hii  kuenzi jitihaba za Mama Maria Kamm katika kuhamasisha wanawake kushiriki katika Masomo ya sayansi wanapokuwa mashuleni, jambo ambalo limesaidia kuongeza idadi ya watafiti wa Kisayansi nchini na hata NIMR.
Mama Maria Kamm alikuwa Mwalimu Mkuu maarufu wa Shule ya Sekondari wa Wasichana ya Weruweru ambaye alibobea katika miaka ya 1970, kwa umahiri wake katika kazi na kwa kuzingatia maadili halisi ya kazi ya ualimu.
Mama kamm alikwa ni miongoni mwa walimu wachache kwa kipindi hicho waliopata Shahada ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Notre Dame.
Tunamuenzi Mama Maria Kamm kwa juhudi zake katika kuzalisha wanawake watafiti na viongozi katika sekta mbalimbali jambo ambalo limechangia kuinua uwezo wa wanawake katika kuongoza na kuleta maendeleo ya jamii.
4.   Professor Wenceslaus Kilama Best Upcoming Award
Tuzo hii inalenga kumuenzi aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Kwanza wa NIMR katika miaka ya themanini Professor Wenceslaus Kilana ambaye alikuwa mchapa kazi na aliyependa kupima matokeo  halisi ya kazi za wanasayansi sambamba na uwezo wa mwanasayansi katika kuvumbua mambo mapya kupitia utafiti, na hasa kwa kwa wanasayansi chipukizi.
Tuzo hizi zitakuwa zikitolewa kila mwaka katika kongamano hili la Kisayansi
 
Ndugu Wanahabari,
Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha taasisi mbalimbali za serikali na waandishi wa Habari wanaoviwakilisha vyombo vya Habari vilivyopo mkoani Arusha kuhudhuria kongamano hili, ili kupata taarifa mbalimbali za utafiti hatimaye kuweza kutoa taarifa hizo kwa Watanzania na kukuza weledi wa jamii kuhusu mbinu za kuimarisha afya ya binadamu kupitia utafiti. 

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

No comments:

Post a Comment