July 23, 2011

R.I.P DANNY MWAKITELEKO

Danny Mwakiteleko
MHARIRI wa gazeti la Rai, ambaye pia ni Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari, Danny Mwakiteleko , amefariki dunia.

Habari ambazo blogu hii imezipata leo alfajiri na kuthibitishwa na watu wa karibu zinasema kwamba Mwakiteleko amefariki leo alfajiri katika hoispitali ya Muhimbili.

Mwakiteleko alilazwa katika kitengo cha watu mahtuti Muhimbili baada ya ajali aliyoipata juzi usiku (jumatano) eneo la Tabata (ToT) na kukimbizwa katika Hospitali ya Amana, Ilala na baadaye Muhimbili.
Katika ajali hiyo gari alilokuwa akiendesha Mwakiteleko liligongwa na lori lenye trela, ambalo lilitoweka bila kujulikana saa nne usiku. Mwakiteleko alikuwa akitokea kazini Sinza ambako alifanya kazi hadi saa tatu usiku.

Mwakiteleko alipelekwa katika Hospitali ya Amana kwa uangalizi hadi saa 12 asubuhi, ambapo madaktari waliamua apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Baada ya uchunguzi Muhimbili, madaktari walisema majeruhi alikuwa ameumia kichwani na kumfanya apoteze fahamu kiasi (semi-conscious) hivyo ikabidi apelekwe katika chumba cha upasuaji ambako madaktari walimhangaikia kuanzia saa sita hadi saa tisa mchana.

Jana Rais Jakaya Kikwete alienda kumuona na kuelezwa kwamba hali yake inaendelea vyema. BLOG hii inawapa pole wafiwa wote hasa familia ya Marehemu.
 Danny Mwakiteleko (kulia) akiwa katika picha pamoja na wanachama wenzake wa Jukwaa la Wahariri pamoja na waandishi wa habari wa mkoani Arusha hivi karibuni.
 Mwakiteleko akiwa katika foleni ya kuchukua chakula katika picha iliyopigwa Julai 15, 2011 saa 3:02 jioni baada ya kumaliza sehemu ya kwanza ya mkutano wao katika hoteli ya Kibo Palace mjini Arusha.
 Alikuwa ni mtu wa kufurahi wakati wote na hapa alikuwa akifurahia mzaha uliokuwa ukifanywa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri TEF, Absalom Kibanda (kushoto) pamoja na Wahariri Joseph Kulangwa wa Habarileo(wapili kushoto) na Mhariri wa Nipashe
 Danny Mwakiteleko huenda hiki ndio kilikuwa cheti chake cha mwisho kupokea hapa duniani na aliyebahatika kumkabidhi cheti hicho ni Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya Bia Serengeti Teddy Mapunda. Hii ilikuwa siku ya mwisho ya Mkutano wa Jukwaa la Wahariri mjini Arusha. Julai 16,2011.Wengine katika picha hiyo ni Mwenyekiti Absalom Kibanda (kushoto) Salim Said Salim na Neville Meena Katibu wa Jukwaa.
Ni mtu wa kujichanganya pia alikuwa na hata panapotokea furaha kama hivi, wakati wa safari watu walijikusanya kwa haraka na kupiga picha ya furaha. Mwakiteleko ni wa 5 kutoka kulia waliosimama mstari wa nyuma.
Hapa ni Wahariri walipotembelea Kiwanda cha Bia cha Serengeti Mjini Arusha. Hakika msiba huu ni mkubwa sana kwa Tasnia ya Habari nchini hasa ukizingatia ni siku chache tu zimepita Tangu kufariki kwa Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Sozzy Mahmoud. Kundi hili la Wahariri litamkumbuka sana Mwakiteleko na Wanahabari kwa ujumla. Sisi tulimpenda lakini Mungu amempenda zaidi Jina la Bwana Lihimidiwe.

No comments:

Post a Comment