July 08, 2008

Alhaji Mintanga afikishwa Mahakamani leo

Aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania, Shaaban Mintanga, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kufikishwa akikabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama za kusafirisha dawa za kulevya kutoka Tanzania kwenda Mauritius na kushiriki katika tukio hilo.

Akisomewa mashtaka yake na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Charles Kenyela, Rais huyo anadaiwa kuwa Juni 3, mwaka huu, alikula njama akiwa na wenzake sita na kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 4.8 zenye thamani ya milioni 120 kutoka Tanzania hadi Mauritius.

Aidha, Kenyela alidai kuwa katika shtaka la pili, Mintanga anadaiwa kuwa Juni 10, mwaka huu alisafirisha dawa hizo kwa kushirikiana wenzake hao sita, hata hivyo alikana mashtaka yote mawili.

Mintanga alirudishwa rumande huku akiwa amekosa dhamana kutokana na kesi yake kutokuwa na ruhusa ya kutopewa dhamana.

Kenyela alidai mbele ya Hakimu Mkazi Euphemia Mingi, kuwa Mshitakiwa huyo hawezi kupewa dhamana kwani sheria inaeleza wazi kesi yoyote inayohusiana na dawa za kulevya na makosa ya jinai haitapewa dhamana kwa mujibu wa sheria.

“Upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika kwani kuna watuhumiwa wengine sita wanategemewa kuungana na mshitakiwa ili watoe uwamuzi” alidai Kenyela.

Kesi hiyo itatajwa tena julai 16 mwaka huu.

Mintanga alikamatwa wiki iliyopita na kushikiliwa katika kituo cha kati akihusishwa na sakata la mabondia waliokamatwa na dawa za kulevya Mauritius.

2 comments:

  1. AnonymousJuly 10, 2008

    Yeye sio wa kwanza na wala sio biashara yake peke yake. Wapo wengi wameanza na hawakamatwa bahati mbaya tu yeye yamempata. Kweli mbio za sakafuni huishia ukingoni

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 10, 2008

    Ndio maana mabondia wengine huwa hawachukuliwi hasa wa mikoani kwa visingizio vya kiwango kumbe kuna kazi mbili mbili wanahitaji kufanya. MMH! Bado riadha tusubiri

    ReplyDelete