Nafasi Ya Matangazo

June 15, 2024


Mwenyekiti wa Shirila la Stemm Afrika Lazaro Nyalandu akitoa taarifa kuhusu kambi ya matibabu ya Siku Tano ya madaktari bingwa kutoka Marekani, Zimbabwe na Tanzania inayofanyika Kijiji cha Pohama wilaya ya Singida.
Kazi ya matibabu ikiendelea kwa wananchi waliojitokeza.
Kazi ya matibabu ikiendelea kwa wananchi waliojitokeza.
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali mkoani Singida na Mikoa ya jiraji wakiwa wamejitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata matibabu ya kibingwa.
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akipatiwa ufafanuzi wa matibabu na Mwenyekiti wa Shirila la Stemm Afrika Lazaro Nyalandu.
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akisalimiana na Manusura wa ajali ya basi la shule ya St Lucky Vicent ambao wamekuja nchini kwa ajili ya kujitolea kutoa matibabu kwa wananchi katika kijiji cha Pohama Halmashauri ya Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza na Wananchi waliojitokeza kupata matibabu ya kibingwa kutoka kwa Madaktari bingwa kutoka Marekani na Zimbabwe katika kijiji cha Pohama wilayani Singida.
Mwenyekiti mwenza wa Shirika la Stemm kutoka Marekani Steven Mayor akizungumza katika uzinduzi wa Matibabu ya Kibingwa bure kwa wananchi wa Kijiji cha Pohama wilayani Singida

Wanafunzi Watatu walionusurika katika ajali mbaya ya basi la shule ya St Lucky Vincent iliyotokea mwaka 2017 na kuua wanafunzi 32 wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa msaada aliyowapatia kwa Ushirikiano na Shirika la Kimataifa la linalojishughulisha na utoaji wa Matibabu kwa Wananchi la Stemm kwenda kupata matibabu ya kibingwa na bobei nchini Marekani.

Vijana Hao Sadhia Awadhi, Wilson Tarimo na Doreen Mshana wametoa shukrani hiyo katika Kijiji cha Pohama wilayani Singida katika uzinduzi wa Kambi ya Matibabu inayofanywa na Madaktari Bingwa kutoka nchini Marekani, Zimbabwe na Tanzania  wakiwa ni Vijana wanaojitolea kuja nchini kwa ajili ya kusaidia wananchi kupatia matibabu ya kibingwa na bobezi bure.

Wamekiri kuwa bila jitihada za makusudi za Rais Samia ambaye kipindi hicho Alikuwa ni Makamu wa Rais ingekuwa ni vigumu mno kwa wao kwenda kupata matibabu ya kibingwa nchini Marekani hali ambayo ilimewasaidia kupona na sasa ni wazima na wenye afya njema.
Vijana hao wamesema baada ya kupona kwa sasa wamepata ufadhili kwa kusomeshwa na Shirika la Stemm na wanaendelea na masomo yao katika Chuo cha Klesten Iowa nchini Marekani.

Akizungumza katika uzinduzi wa kambi ya Matibabu bure ambayo inatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi 3000 katika Kijiji cha Pohama wilaya ya Singida, Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego amemshuruku Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada alizozifanya mpaka Vijana hao waliopata ajali na kwenda kupatiwa matibabu bure nchini Marekani na kusema hilo ni jambo kubwa na la mfano kwa jamii nzima ya Watanzania.

Halima Dendego amesema mahusiano mazuri yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na Mataifa mengine ya nje ndio yanachangia kwa kiasi kikubwa kumiminika kwa misaada mbalimbali ikiwemo katika sekta ya afya.

Amewasisitiza Watanzania kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika uimarishaji wa huduma kwenye sekta mbalimbali na waache kumkatisha tamaa kwa sababu Rais ana maono makubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo makubwa na endelevu.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amewashukuru Madaktari Bingwa kutoka Marekani na Zimbabwe kwa kuja nchini kwa ajili ya kuja kutoa matibabu bure ya kibingwa kwa Watanzania hasa maeneo ya vijijini jambo ambalo linasaidia wananchi kutosafiri umbali mrefu kwenda kufuata huduma hizo hasa kwenye Hospitali za Rufaa.

Naye, Waziri wa Zamani wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika la Stemm kwa Upande wa Afrika amesema jitihada za Rais Samia za kusaidia Watanzania kupata huduma bora za afya ndio zimewavuta Wadau wa Maendeleo wa Kimataifa kuja nchini kutoa matibabu bure kwa wananchi.

Lazaro Nyalandu amesema yeye na Wadau wengine wa Maendeleo wataendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kutoa misaada wa hali na mali ili kuhakikisha utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za afya zinaimarika maradufu mijini na Vijijini ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi wakiwa na afya njema.
Posted by MROKI On Saturday, June 15, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo