Nafasi Ya Matangazo

May 24, 2024

Na Eleuteri Mangi, WANMM, Dodoma
Waziri wa Ardhi, Nyumba ya Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa ametaja vipaumbele vitano vya wizara hiyo kuwahudumia Watanzania sekta ya ardhi nchini kwa mwaka 2024/2025 na kuliomba Bunge lijadili na kuidhinisha ni Shilingi 171,372,508,000 ili kutekeleza majukumu ya wizara hiyo

Akiwasilisha Bungeni Hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Mei 24, 2024 jijini Dodoma, Waziri Silaa amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi mijini na vijijini, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma na upatikanaji wa taarifa za ardhi.

Vipaumble vingine ni kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuimarisha mipaka ya kimataifa.

“Nawahimiza wananchi kote nchini kuendelea kutumia Ofisi za Ardhi za Mikoa kupata huduma za umilikishaji wa ardhi na kuhakikisha wanamilikishwa maeneo yao kwa mujibu wa sheria” amesema Waziri Silaa.

Miongoni mwa majukumu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo yatafanikisha vipaumbele vya wizara hiyo ni kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi, kusimamia upangaji wa miji na vijiji, kupima ardhi na kutayarisha ramani, kutoa hati za kumiliki ardhi na hatimiliki za kimila, kusajili hati za umiliki ardhi na nyaraka za kisheria pamoja na kuthamini mali. 

Majukumu mengine ni kuhamasisha na kuwezesha wananchi kuwa na nyumba bora, kutatua migogoro ya ardhi na nyumba, kusimamia upatikanaji na utunzaji wa kumbukumbu za ardhi, kusimamia ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yatokanayo na huduma za sekta ya ardhi, kusimamia Shirika la Nyumba la Taifa, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi na Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni, kusimamia uendeshaji wa Vyuo vya Ardhi vya Tabora na Morogoro na, kusimamia maslahi na utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya ardhi.

Aidha, Waziri Silaa amewapongeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kwa ushirikiano wao wa karibu kwa Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa na wataalamu wa sekta ya ardhi katika kuendesha na kusimamia Kliniki za ardhi katika maeneo yao.
Posted by MROKI On Friday, May 24, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo