Nafasi Ya Matangazo

April 22, 2024







Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa uhifadhi, Frankfurt Zoological Society (FZS) kutoka Ujerumani na Six Rivers Africa (SRA) ya Tanzania ambao wamekuwa wakiisaidia Serikali katika maeneo mbalimbali ya uhifadhi ikiwemo urejeshaji wa wanyama waliotoweka (restoration),utafiti, kupambana na ujangili na kusaidia jamii kujikwamua kiuchumi hasa zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi pamoja na masuala ya utalii.

Kikao hicho kimefanyika leo Aprili 22,2024  katika ukumbi wa hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kairuki ameendelea kuwaomba ushirikiano katika uhifadhi ikiwemo ufuatiliaji wa idadi na kufanya sensa ya wanyamapori katika mifumo ikolojia mingine ambayo muda wa sensa ya wanyamapori umechelewa akitolea mfano wa ikolojia za Burigi-Chato, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Malagarasi-Moyowosi-Kigosi na Serengeti.


Pia, amewaomba wadau hao kushiriki katika kujengea uwezo wahifadhi hasa kuhusu maendeleo ya teknolojia katika kufanya sensa ya wanyamapori na kununua vifaa vilivyoboreshwa vya ufuatiliaji wa wanyamapori na kutoa ufadhili katika tafiti za aina muhimu za Wanyamapori wakiwemo Faru, Tembo, Wanyama Wanyama Wakubwa (Simba, Chui, mbwa mwitu).

Katika hatua nyingine, amewaomba ushirikiano katika kuimarisha teknolojia kwenye kupunguza mwingiliano baina ya Binadamu na Wanyamapori ili kupunguza madhara yanayotokea kwa wananchi, kusaidia katika zoezi la urejeshaji wa shoroba za wanyamapori na kuimarisha teknolojia katika ufugaji nyuki katika maeneo yanayozunguka Hifadhi za Serengeti na Nyerere kwa ajili ya maisha ya jamii na kuboresha miundombinu (nyumba, doria barabara na viwanja vya ndege).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amewashukuru wadau hao kwa namna ambavyo wamejitolea katika uhifadhi na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uhifadhi wanayoiendesha.

Wadau hao kwa nyakati tofauti wamesema wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uhifadhi, utafiti na kuboresha maisha ya jamii zinazopakana na Hifadhi.

FZS na SRA wamekuwa wakisaidia shughuli za uhifadhi wa Faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Grumeti-Ikorongo, Pori la Akiba la Maswa na Hifadhi ya Ngorongoro, ufuatiliaji wa idadi ya wanyamapori (sensa) katika mfumo ikolojia wa Serengeti na mfumo wa ikolojia wa Selous-Nyerere-Mikumi na kusaidia shughuli za Utafiti.
Posted by MROKI On Monday, April 22, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo