Nafasi Ya Matangazo

December 22, 2016



Katibu Mkuu kiongozi Balozi John Kijazi akitangaza uteuzi wa viongozi ya Tume ya Uchaguzi, Tume ya Maadili  na Majaji wa Mahakama ya Rufaa Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 22, 2016.
********************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 22 Desemba, 2016 amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jaji Semistocles Kaijage kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Jaji Semistocles Kaijage ameteuliwa kuongoza Tume hiyo kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.

Mhe. Jaji Semistocles Kaijage anachukua nafasi ya Mhe. Jaji Mstaafu Damiani Lubuva ambae muda wake wa kuwa Mwenyekiti umemalizika rasmi mnamo tarehe 19 Desemba, 2016.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mahamoud Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kipindi kingine cha miaka 5 kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.

Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mahamoud Hamid alikuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC na amemaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka 5 mnamo tarehe 19 Desemba, 2016.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli pia amemteua Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jaji Harold Reginald Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016. 

Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Jaji Mstaafu Salome S. Kaganda ambae amestaafu mnamo tarehe 10 Desemba, 2016.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amewateua Majaji 4 wa Mahakama Kuu kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani kuanzia leo tarehe 22 Desemba, 2016 kama ifuatavyo:-

i)    Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika
ii)   Mhe. Jaji Jackobs Mwambegele
iii)  Mhe. Jaji Rehema Kiwanga Mkuye
iv)   Mhe. Jaji Sivangilwe Sikalalilwa Mwangesi

Wateule wote waliotajwa katika taarifa hii wataapishwa kesho Ijumaa, tarehe 23 Desemba, 2016 saa 3:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Posted by MROKI On Thursday, December 22, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo