Nafasi Ya Matangazo

February 07, 2010

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akipokea mfano wa hundi ya shs milioni 50 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Dietlof Mare (wa pili kushoto) zilizopatikana kupitia kampeni ya Vodafone Red Alert kwa ajili ya maafa yaliyotokea Same na Kilosa. Hafla hiyo ilifanyika katika makazi ya waziri Pinda, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wengine kutoka kushoto ni Mwamvita Makamba wa Vodacom, Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba kutoka Clouds FM.

KAMPUNI ya simu za mikononi ya Vodacom Tanzania mwishoni mwa wiki ilimkabidhi Waziri Mkuu Mizengo Pinda hundi ya Milioni 50/- zilizokusanywa na kampeni ya kusaidia jamii ya kampuni hiyo ‘Vodafone Red Alert’ ambazo zitatumika kuwasaidia waathirika wa mafuriko nchini.
Vodacom ilizindua kampeni hiyo inayoendeshwa takribani nchi 27 za Afrika baada ya kuguswa na maafa kutokana na mafuriko yaliyowakumba wakazi wa maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Kilosa, Same, Arusha, Mtwara, Ngerengere na kusababisha vifo na uharibifu wa mali zikiwemo nyumba.

Akipokea hundi hiyo Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa atahakikisha msaada huo unatumika kwa lengo lililokusudiwa kwani watu wengi wameathirika na maafa hayo ya mafuriko na kwamba Kilosa peke yake watu 28,000 wameathirika.

Hata hivyo aliishukuru kampeni hiyo ya Vodafone Red Alert iliyoendeshwa na Vodacom Tanzania wakishirikiana na CloudsFm, asasi za kiraia na taasisi za kidini kwa kujitokeza kuwachangia waathirika na kutumia fursa hiyo kuzitaka kampuni zingine kujitokeza kuunga mkono mpango huo.

“Naishukuru kampuni ya Vodacom na Watanzania wote waliojitokeza kuchangia, na kwamba kampuni zingine ziige mfano huu utakaowezesha kuzisaidia jamii zilizoathirika na mafuriko kote nchini kwani misaada bado inahitajika,” alisema Pinda.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Dietlof Mare alisema kampuni yake kupitia kampeni ya Vodacom Red Alert itaendelea kuisaidia jamii ya Watanzania pale yatakapojitokeza maafa mengine kote nchini.

Aidha alisisitiza kuwa bila ya ushirikiano wa wateja wapatao milioni saba wa Vodacom Tanzania zoezi hili lisingefanikiwa. Hivyo aliwashukuru wateja wa Vodacom na wananchi wengine waliojitokeza kuchangia misaada mbalimbali na kuitikia wito wa kampuni hiyo uliokuwa na lengo la kuwasaidia Watanzania wenzao.

“Baadhi ya wananchi walijitokeza kuchangia misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo magodoro, nguo, sabuni na bidhaa nyinginezo. Lakini kubwa zaidi nawapongeza wateja wa Vodacom kwa kuchangia kiasi hicho cha milioni 50/-,” alisema Mare.

Kampeni hiyo ya Vodafone Red Alert iliyozinduliwa Januari 24 ilikamilika Februari 1. Ili kuwachangia wahanga, wateja wa Vodacom walipaswa kutuma ujumbe wenye neno MAAFA au REDALERT kwenda namba 15599, kila ujumbe ulikuwa ukigharimu 250/- pamoja na VAT.
Akizindua kampeni hiyo, Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Vodacom Tanzania, alisema kampeni hiyo ilikuwa ni muhimu katika kuyarejesha kwenye hali ya kawaida maisha ya Watanzania walioathiriwa na maafa katika sehemu mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya VODACOM Tanzania na Radio ya Clouds waliofanikisha ukusanyaji wa michango ya zaidi ya Shilingi milioni 50 na vitu mbalimbali kwa ajili ya waliopatwa na maafa ya mafuriko wilayan i Kilosa . Mheshimiwa Pinda alikabidhiwa vitu na fedha hizo na viongozi wa VODACOM na Radio ya Cloud, kwenye makazi yake jijini Dar es salaam, Februari 7, 2010.
Posted by MROKI On Sunday, February 07, 2010 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo