October 28, 2026

KITWIMA YOUTH GROUP, SHAMBA DARASA KWA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UCHUMI

Na: Dk. Reubeni Lumbagala
Serikali ina vipaumbele vingi vya maendeleo kwa ajili ya watu wake. Miongoni mwao ni uwezeshaji wananchi kiuchumi. Hapa serikali huweka mazingira rafiki na wezeshi kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanatumia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo ili kujiongezea kipato na kuchangia maendeleo ya nchi.

Katika juhudi za maendeleo, kundi la vijana ni muhimu kuwezeshwa ili nao washiriki kikamilifu katika maendeleo. Vijana wana nguvu na maarifa ya kuweza kuzalisha na hatimaye kubadili hali zao za maisha kutoka hali duni na kuwa nzuri zaidi. Ni kundi ambalo likiwezeshwa, maendeleo yatasonga mbele kwa haraka zaidi.

Kutokana na umuhimu wa kundi la vijana katika maendeleo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameanzisha wizara maalum ya kushughulikia masuala ya vijana - Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana chini ya uongozi wa Waziri wake, Joel Nanauka.

Wizara hii hajachanganywa na sekta nyingine yeyote, imebaki kushughulikia masuala ya maendeleo ya vijana. Basi. Huu ni upekee wa aina yake kutokana na dhamira ya serikali ya kuhakikisha kundi la vijana linakamata fursa muhimu za uchumi kwa maendeleo.

Katika kuhakikisha uwezeshaji vijana kiuchumi haubaki kuwa mpango wa kwenye makaratasi tu, serikali ikaweka katika vitendo kwa kutoa shilingi bilioni 200 ili zikopeshwe kwa vijana bila riba. Fedha hizi zikawekewa utaratibu kwa vijana katika vikundi waungane na watume maombi na kwa wale watakaokidhi vigezo watakopeshwa.

Kikundi cha vijana cha Kitwima yaani Kitwima Youth Group (KYG) ni miongoni mwa wanufaika wa mkopo wa shilingi bilioni 200 zilizokopeshwa na vijana nchi nzima. Kikundi hiki ni cha vijana wasomi ambapo wamejikita katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, katika Ziwa Viktoria, mkoani Mwanza.

Ni kwamba, kikundi hiki kilipata mkopo wa shilingi milioni 106.9, mwezi Machi, 2026. Baada ya kupokea fedha hizo, walinunua vifaranga vya samaki 60,000 kwa shilingi milioni tisa, wakaongezwa vifaranga 6,000 na kufanya vifaranga vya samaki kufika 66,000.

Vilevile, walitengeneza keji kwa shilingi milioni 35, wakanunua mtumbwi, chakula cha samaki na majaketi ya kuwasaidia katika shughuli zao za uvuvi (life jackets). Ndani ya miezi saba ya shughuli hiyo (Machi - Oktoba, 2026) wameweza kuzalisha samaki tani 15 aina ya Sato ambao mauzo yake yana thamani ya shilingi milioni 127.5.

Kimsingi, kikundi hiki kimeonyesha uthubutu mkubwa na kimetoa darasa kwa vijana wenzao katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, kuchangamkia fursa za uchumi zinazoratibiwa na serikali. Kupitia mradi huu, vijana hao wamejihakikishia kipato kupitia mauzo ya samaki pindi wanapowavuna.  

Pengine sana, kupitia mafanikio ya kikundi cha Kitwima, vijana waongeze ari ya kufuatilia mikopo inayotokewa na Wizara ya Vijana na Wizara nyingine ili vijana waweze kubadili maisha yao kwa kujiajiri wenyewe. Aidha, waliopewa dhamana ya kushughulikia mikopo ya vijana watende haki, waondoe urasimu ili vijana wanufaike na fursa hizo muhimu kwa maendeleo endelevu.

Maoni : 0620 800 462.

No comments:

Post a Comment