Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Kurugenzi ya Huduma Saidizi na Utawala katika Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), DCC Emmanuel Wilfred Kiboko akitoa mada.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Kurugenzi ya Huduma Saidizi na Utawala katika Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), DCC Emmanuel Wilfred Kiboko, amewaonya watumishi wapya 328 kutokuondoka katika vituo vyao vya kazi bila kufuata utaratibu, akisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
DCC Kiboko ametoa kauli hiyo
leo, Jumanne, Septemba 15, 2026, wakati akiwasilisha mada katika siku ya pili
ya programu ya mafunzo elekezi kwa watumishi hao inayofanyika Dodoma.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Kurugenzi ya Huduma Saidizi na Utawala katika Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), DCC Emmanuel Wilfred Kiboko, amewaonya watumishi wapya 328 kutokuondoka katika vituo vyao vya kazi bila kufuata utaratibu, akisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Amesema
baada ya kukabidhiwa barua za ajira, watumishi hao wanatakiwa kuripoti katika
vituo vyao vya kazi ndani ya siku saba, huku wakuu wa vituo wakitakiwa
kuthibitisha kuripoti kwao na kuwapatia majukumu.
“Ukiondoka kwenye kituo cha
kazi kwa utaratibu wowote ule, ina maana utapaswa kuchukuliwa hatua za
kinidhamu kwa utoro kazini,” amesema DCC Kiboko, akiwataka watumishi hao
kuchukulia kwa uzito masharti ya ajira na taratibu za utumishi wa umma.
Amesema pia watumishi hao
hawataruhusiwa kuondoka vituoni kwenda kumalizia masomo bila kufuata taratibu
na kupata kibali cha Kamishna wa Uhifadhi. Amesema TFS imebaini baadhi ya wakuu
wa vituo wamekuwa wakiwaruhusu watumishi kwenda kumalizia masomo kinyume na
taratibu, na kuwa hatua zinaweza kuwahusu viongozi watakaofanya hivyo bila
kibali.
Akizungumzia mafunzo na
maendeleo ya kielimu, DCC Kiboko amesema TFS hutumia Training Needs Assessment
(TNA) kubaini maeneo ambayo taasisi inahitaji kuwekeza katika mafunzo, huku
Training Programme ikibainisha mahitaji ya kila mtumishi na muda wa mafunzo
kulingana na mahitaji ya taasisi na uwezo wa bajeti.
Amesema ajira za watumishi hao
328 zinalenga kuongeza nguvu kazi katika maeneo ya utekelezaji wa majukumu ya
TFS, hivyo watumishi wanapaswa kutimiza wajibu wao katika vituo walivyopangiwa
ili kufikia matarajio ya Serikali ya kuongeza ufanisi na mapato.
Aidha, amewataka watumishi hao
kujiunga na vyama vya kitaaluma vinavyohusiana na kada zao, akitolea mfano
Tanzania Association of Foresters (TAF) kwa wataalamu wa misitu, huku
akisisitiza kuwa utumishi wa umma ni safari inayoendelea inayohitaji kujifunza na
kukumbushana kuhusu maadili kila siku.
Akihitimisha, DCC Kiboko
amewataka watumishi hao kuzingatia nidhamu, uadilifu na taratibu za utumishi,
akisisitiza kuwa wanapaswa kulinda heshima ya TFS, Utumishi wa Umma, wao
wenyewe na familia zao katika kipindi chote cha utumishi wao.







No comments:
Post a Comment