WANANCHI GEITA WAIPONGEZA JKCI KWA HUDUMA BINGWA NA BOBEZI ZA MOYO
Wananchi wa Mkoa wa Geita
wameishukuru na kuipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa
huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya tisa
ya kitaifa ya tekinologia ya madini.
Pongezi hizo zimetolewa na
wananchi mbalimbali waliofika katika banda la JKCI na kufanyiwa uchunguzi wa
afya ikiwemo kupimwa kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu,
mzunguko wa kiuno, vipimo vya moyo pamoja na uwiano wa uzito kwa urefu.
Rose Egatha mkazi wa Geita mjini
alisema amefika katika banda hilo baada ya kupata taarifa kuhusu uwepo wa
huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa sababu amekuwa akisumbuliwa na
maumivu makali ya kifua ya muda mrefu.
“Nawashukuru sana JKCI kwa kutuletea huduma
hizi kwani zimenisaidia kujua tatizo langu la moyo, kabla ya hapo nilikuwa
nikimeza dawa mbalimbali bila kupima hivyo nashauri wananchi wenzangu tusimeze
dawa bila kupata vipimo na ushauri wa dakatari”, alisema Rose.
Aisha Ramadhani Mkazi wa
kalangalala aliishukuru serikali kwa kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya
moyo karibu na maeneo yao na kuiomba iendelea kuwajali wananchi wanaoishi
maeneo ya pembezoni.
“Hii ni mara yangu ya kwanza
kufika hapa kwani nimekuwa nikisikia kuhusu JKCI kupitia vyombo vya habari hivyo
maonesho haya yamekuwa yakipekee kwangu na yameniletea matumaini makubwa juu ya
afya yangu”, alisema Aisha.
Naye Idrisa Ntarembo Mkazi wa
Nyamalembo alisema amefarijika kupata ushauri wa lishe bora kutoka kwa dakatri
bingwa wa moyo nakuahidi kuufanyia kazi.
“Ushauri niliopewa utanisaidia
kulinda afya ya moyo wangu sambamba na hilo nimepewa dawa za kutibu tatizo la
shinikizo la damu hivyo ningependa kuwashauri wananchi wenzangu watumie fursa
hii ya maonesho kufanya uchunguzi wa afya ili wajue hali zao za kiafaya”,
alisema Idrisa.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) inashiriki katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya tekinolojia ya madini kwa kuwafanyia
wananchi uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo.
No comments:
Post a Comment