September 08, 2026

ORCI YAANZA SAFARI YA ITHIBATI YA KIMATAIFA, YALENGA KUONGEZA UBORA, USALAMA NA IMANI YA WAGONJWA

 Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi Tiba na Uhakiki Ubora wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Hemed Myanza akiwaeleza wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi hatua zilizofikiwa na taasisi hiyo katika mchakato wa kupata ithibati ya ubora wa huduma  wakati wa kikao cha sita cha baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Stella Maris iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani. Picha na ORCI
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi Tiba na Uhakiki Ubora, Hemed Myanza wakati akiwaeleza hatua zilizofikiwa katika mchakato wa kupata ithibati ya ubora wa huduma wakati wa kikao cha sita cha baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Stella Maris, Bagamoyo mkoani Pwani.


Na Mwandishi Maalumu – Bagamoyo
Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) imeanza maandalizi ya kupata ithibati ya ubora wa huduma ikiwa tayari imefanya tathmini katika maeneo mbalimbali na kubaini mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kufikia viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za ORCI za kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza usalama wa wagonjwa na kuhakikisha huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo zinaendana na viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi Tiba na Uhakiki Ubora wa ORCI, Hemed Myanza wakati akieleza hatua zilizofikiwa katika mchakato wa kupata ithibati, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi katika kikao cha sita cha baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Stella Maris wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Myanza alisema  katika maandalizi hayo ORCI imeweka mkazo katika kuhakikisha Taratibu za Kawaida za Uendeshaji (Standard Operating Procedures – SOPs) zinawekwa na kutumika katika maeneo yote ya taasisi ili kuwepo kwa mifumo na viwango vinavyofanana katika utoaji wa huduma.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila eneo la huduma linafanya kazi kwa kuzingatia taratibu na viwango vilivyowekwa jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi, usalama na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.

Aidha Myanza alisema  ORCI tayari imefanya mazungumzo na bodi zinazohusika na ithibati za kimataifa hatua inayolenga kusaidia taasisi kubaini chombo cha ithibati itakachoshirikiana nacho pamoja na kuelekezwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikia kiwango cha kupata ithibati ya kimataifa.

“Tumeshatoa elimu kwa wafanyakazi na tumeweza kuona maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia maboresho. Tumekwenda katika maeneo yote ya kitabibu na yasiyo ya kitabibu ili kuhakikisha watumishi wanakuwa na uelewa mmoja kuhusu viwango vinavyotakiwa kimataifa katika utoaji wa huduma”,  alisema Myanza.

Alisema mchakato huo haujajikita katika maeneo ya kitabibu pekee bali unahusisha pia maeneo yasiyo ya kitabibu ili kuhakikisha watumishi wote wanakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu viwango vinavyopaswa kuzingatiwa katika utoaji wa huduma.

Myanza alisema  huduma kwa wateja (customer care) ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele katika mchakato huo, ambapo ORCI inalenga kuhakikisha watumishi wanakuwa na uelewa na uwezo wa kutoa huduma bora, salama na zenye viwango vya juu vinavyoweza kuendana na viwango vya kimataifa.

Alisema  tathmini zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya taasisi zimewezesha kubaini mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi huku hatua za maboresho zikiendelea ili ORCI iweze kufikia viwango vinavyohitajika.

“Lengo la ithibati ni kuhakikisha taasisi inatambuliwa kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa. Tumefanya tathmini na kubaini maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia maboresho ili kufikia viwango hivyo vya kimataifa”,  alisema.

Myanza alisema kupata ithibati hiyo kutasaidia kuongeza imani na uaminifu wa wagonjwa kwa ORCI kwa kuwa utambuzi huo utaonesha kuwa taasisi inatoa huduma kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika vya ubora na usalama.

“Tunatarajia ithibati hii itaongeza imani na uaminifu wa wagonjwa kwa sababu watakuwa na uhakika na kuthamini zaidi huduma wanazozipata katika taasisi yetu”, alisema.

Kwa upande wao wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi waliupongeza uongozi wa ORCI kwa hatua mbalimbali za maboresho yanayolenga kuongeza ubora wa huduma na kuimarisha mazingira ya kazi huku wakisisitiza umuhimu wa kuunganisha uwekezaji katika miundombinu na vifaa vya kisasa na mifumo madhubuti ya utoaji wa huduma bora.

Naye Wamoja Mbonde ambaye ni Msimamizi wa Kumbukumbu za Afya na Mjumbe wa Baraza hilo alisema  kupata ithibati kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa na ORCI kwa kuwa kutaiwezesha taasisi kuwa na mifumo na viwango vinavyofanana katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma.

Alisema  ithibati hiyo pia itasaidia kuimarisha uwajibikaji wa watumishi, kuzingatia taratibu na viwango vilivyowekwa pamoja na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa zinaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia mahitaji na usalama wao.

“Uwepo wa ithibati utasaidia kuhakikisha tunafanya kazi kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwani kila mfanyakazi atavituata kwa vitendo, wagonjwa wataona tofauti katika huduma wanazopata. Hii itaongeza imani yao na kuifanya ORCI kuwa taasisi inayozingatia ubora katika kila hatua ya huduma”, alisema Mbonde.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani na Mjumbe wa Baraza hilo Faraja Kiwanga alisema mchakato wa kupata ithibati unapaswa kwenda sambamba na maboresho ya miundombinu, vifaa na mashine za kisasa yanayoendelea katika  taasisi hiyo ili uwekezaji unaofanyika uweze kuleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.

Dkt. Faraja alisema  maboresho hayo yakitekelezwa sambamba na mifumo madhubuti ya ubora na watumishi kuzingatia viwango vilivyowekwa, yataendelea kuongeza uwezo wa ORCI katika kutoa huduma bora, salama na zenye ufanisi kwa wagonjwa kutoka ndani na nje ya nchi.

Kupatikana kwa Ithibati kutaifanya  ORCI kuwa na mifumo thabiti ya ubora katika maeneo yote ya utoaji wa huduma,  kuongeza uwajibikaji wa watumishi, usalama wa wagonjwa na imani ya wananchi katika huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.

No comments:

Post a Comment