Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya mikutano miwili ya pande mbili (bilateral meetings) pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 70 wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA) Jijini Vienna, Austria, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tanzania kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Katika mkutano wake na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Bw. Rafael Mariano Grossi, mazungumzo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani na maendeleo, hususan matibabu ya saratani, kilimo na usalama wa chakula, lishe, maendeleo ya wataalamu pamoja na maandalizi ya Tanzania kuelekea matumizi ya nishati ya nyuklia kama nyongeza ya vyanzo vya uzalishaji umeme nchini siku zijazo.
Aidha, Makamu wa Rais amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Vienna (UNOV) na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Dkt. Monica Juma. Mazungumzo yaliyolenga kuendeleza ushirikiano baina ya Tanzania na UNODC katika juhudi za kudhibiti dawa za kulevya.
Makamu wa Rais, Mhe. Ndejembi, yuko Jijini Vienna, Austria, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Mkuu wa 70 wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA), unaowakutanisha Viongozi na Wawakilishi wa Nchi wanachama kujadili masuala mbalimbali yanayohusu matumizi salama na ya amani ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.








No comments:
Post a Comment