Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Tan Communication Media Ltd, inayomiliki na kuendesha kituo cha redio cha Redio 5 cha jijini Arusha, Robert Lowassa, amesema mshikamano baina ya Marekani na Tanzania yaongeze fursa zaidi za uwekezaji nchini.
Lowassa ameyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Msemaji na Afisa Habari wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Nice Cole ofisini kwake Arusha.
Amesema Marekani imekuwa mshirika muhimu kwa Tanzania katika maeneo mbalimbali, ikiwemo utalii, biashara, uwekezaji na miradi ya maendeleo.
Lowassa amesema ni matumaini yake kuwa mshikamano huo utaendelea kuwa imara zaidi ili kufungua fursa nyingi zaidi za uwekezaji na maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TanMedia, Angela Maina, amekaribisha ushirikiano huo, akisema Arusha na Tanzania kwa ujumla vina nafasi kubwa ya kunufaika zaidi kupitia mafunzo kwa vijana na waandishi wa habari, pamoja na programu za kubadilishana uzoefu (exchange programs) zitakazosaidia kukuza taaluma ya habari na uendeshaji bora wa vipindi.
Akizungumza na Radio 5, Msemaji na Afisa Habari wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Nice Cole, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kwa miaka mingi umechangia maendeleo na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili, pamoja na kuimarisha usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema, Marekani inaendelea kuthamini uhusiano wake wa muda mrefu na Tanzania, huku ushirikiano katika sekta za usalama, biashara na uwekezaji, afya pamoja na maendeleo ukiendelea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu katika mahusiano ya nchi hizo mbili.
Katika mahojiano hayo, Cole pia amesema Tanzania inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kujenga minyororo ya usambazaji wa bidhaa na malighafi duniani, kutokana na upatikanaji wa madini muhimu yanayotumika katika sekta mbalimbali.
Amesema Marekani kwa sasa inaangalia kwa karibu suala la critical minerals, akieleza kuwa baadhi ya madini yanayopatikana Tanzania yanaweza kutumika katika sekta ya usafirishaji, ikiwemo uzalishaji wa betri za magari ya umeme.




No comments:
Post a Comment