Na Jeston Kihwelo, Ruvuma
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuchukua hatua za kisera na kiteknolojia kuboresha huduma za ardhi nchini, ambapo matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi yameelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuongeza ufanisi, uwazi na usalama wa taarifa za ardhi.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mfumo huo mkoani Ruvuma, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Ruvuma Bw. Saidi Juma, amesema e-Ardhi imeleta suluhisho la kisasa katika usimamizi na utoaji wa huduma za ardhi, hususan katika kudhibiti changamoto ya double allocation, ambapo eneo moja linaweza kutolewa kwa watu zaidi ya mmoja.
Amesema mfumo huo unawawezesha wataalamu wa ardhi kufanya kazi kwa kutumia taarifa zilizopo kwenye mfumo wa kidijiti, hivyo kurahisisha utambuzi na uhakiki wa taarifa za maeneo kabla ya hatua za utoaji wa huduma kuchukuliwa.
“Mfumo wa e-Ardhi umekuja kurahisisha huduma za ardhi, kusaidia kuondoa changamoto ya double allocation na kumpunguzia mwananchi muda pamoja na gharama za kufuatilia huduma za ardhi,” amesema Saidi Juma.
Aidha, matumizi ya mfumo huo yanaendelea kuimarisha mwelekeo wa Serikali wa kutumia teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wananchi, kwa kupunguza utegemezi wa mifumo ya kawaida ya ufuatiliaji wa huduma na kuweka mazingira ya huduma kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande mwingine, mfumo wa e-Ardhi unatarajiwa kuongeza urahisi kwa mwananchi katika kupata huduma bila kulazimika kusafiri mara kwa mara kufuata huduma katika ofisi za ardhi, hatua inayosaidia kupunguza gharama na muda wa mwananchi.








No comments:
Post a Comment