WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema
ndani ya wiki moja, Serikali itachukua hatua ya kuhakikisha bei ya saruji
inakuwa himilivu kwa wananchi, baada ya kubaini malalamiko ya kupanda kwa bei
ya bidhaa hiyo katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Simiyu.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Septemba 15,
2026) wakati akizungumza na wananchi wa Bariadi Mjini, mkoani Simiyu katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM Saba Saba.
“Serikali tumeliona hilo. Serikali sikivu
tumesikia hilo. Nimewatuma wataalamu ndani ya wiki moja wawe wameshapata
ufumbuzi. Tutatoa tamko la njia ya kushusha bei ya saruji ili kila Mtanzania
aweze kumudu. Katika baadhi ya maeneo bei ya saruji imefikia zaidi ya sh.
26,000 na katika baadhi ya mikoa ya mipakani imefikia sh. 32,000,” amesema na
kusisitiza kuwa Serikali inataka wananchi waweze kumudu gharama za ujenzi wa
nyumba na miradi mingine ya maendeleo.
Kuhusu zao la pamba, Waziri Mkuu amesema
ameielekeza Wizara ya Kilimo ikutane na wadau wa pamba ndani ya mwezi mmoja na
ifikapo Oktoba 15, 2026 apelekewe mapendekezo rasmi kuhusu bei na mfumo bora wa
ununuzi wa zao hilo ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi.
“Nimeipokea hoja hii. Nimeelekeza Wizara ya
Kilimo ikae na wadau wa pamba ndani ya mwezi mmoja. Ifikapo tarehe 15 mwezi wa
10, niwe nimeshapata mapendekezo rasmi yaliyorejea mifumo ambayo tumeshaitumia
na kubaini upi ni mfumo bora ili tuweze kuhakikisha kwamba wakulima
wananufaika,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema
pia Serikali imebadilisha utaratibu wa kodi kwa wenye biashara mpya, ambapo
mfanyabiashara anayeanzisha biashara atapewa muda wa kuimarisha biashara yake
kabla ya kuanza kubeba mzigo wa kodi. “Zamani ilikuwa mtu akianzisha tu
biashara, siku hiyo hiyo anaanza kudaiwa kodi. Sasa tumefuta, atasubiriwa mwaka
mzima ili biashara yake iimarike,” amesema.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji
wa Dira ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kujenga uchumi shirikishi, ambapo sekta
binafsi inatarajiwa kutekeleza sehemu kubwa ya shughuli za maendeleo.
Mapema, akizungumza katika mkutano huo,
Mbunge wa Bariadi Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo
Andrea Mathew, amemshukuru Waziri Mkuu kwa ziara hiyo na kueleza kuwa Serikali
imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo
inayogusa sekta za maji, elimu, afya na barabara.
Mhandisi Kundo amesema mradi mkubwa wa maji
kutoka Ziwa Victoria wenye thamani ya sh. bilioni 440 unaendelea kutekelezwa
mkoani humo, huku Serikali ikiwa imetoa sh. milioni 460 kupitia TARURA kwa
ajili ya ujenzi wa daraja la Majaida–Munambala katika Mto Ndoba.
Kuhusu ujenzi wa soko la kisasa la Bariadi
mjini, Mhandisi Kumndo amesema ujenzi wake unaendelea, huku akiomba kasi ya
mkandarasi iongezwe ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Akigusia barabara za Bariadi Mjini, Mhandisi
Kundo amesema Serikali imeweka mpango wa kuhakikisha kilomita zote 8.6
zilizotengewa ujenzi zinajengwa kwa awamu mbili, ambapo kilomita tano
zitajengwa katika awamu ya kwanza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said
Mtanda, amesema Serikali ya Mkoa itasimamia na kutekeleza maelekezo yote
yaliyotolewa na Waziri Mkuu wakati wa ziara hiyo na kuwasilisha taarifa ya
utekelezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Maagizo na maelekezo yako uliyoyatoa katika
ziara yako hii tunayasimamia, tuyatekeleze, na kuleta ripoti ya utekelezaji
katika ofisi yako ya Waziri Mkuu,” amesema.
No comments:
Post a Comment