August 12, 2026

JARIBIO LA KWANZA LA ZAO LA VIAZI MVIRINGO MKOANI DODOMA LAONYESHA MAFANIKIO MAKUBWA



Dodoma
Jaribio la kwanza la Mbegu ya viazi mviringo lililotafitiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) limeonesha mafanikio makubwa mkoani Dodoma katika shamba la Makamu wa Rais Mstaafu  Mhe. Dkt Philip Mpango lililopo Kijiji cha Mayamaya, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Jaribio hilo lililochukua  siku 104 za majaribio shambani hadi kuvuna limedhihirisha kuwa zao la viazi mviringo linaweza kustawi katika mazingira ya  Mkoa wa Dodoma na kuufanya Mkoa huo kuwa na fursa mpya ya zao la chakula na biashara ambalo linaweza kuwasaidia wananchi wa mkoa huo kuondokana na umasikini.

Akiongelea  kuhusu jaribio hilo na matokeo yake,  Makamu wa Rais  Mstaafu Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameishukuru TARI kwa kusimamia jaribio hilo ambalo kwa mara ya kwanza limeonyesha mafanikio  katika Kijiji cha Mayamaya na kuwataka wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo pindi utafiti utakapokamilika.

“ Wakazi wa  Dodoma sasa tuanze kuchangamkia hii fursa na TARI wako tayari kutusaidia kwa kutupatia mbegu bora zinazofaa zaidi na hii itatusaidia chakula na kipato kwa ajili ya kusaidia watoto wetu kwenda shule. Dodoma sio nusu jangwa, ni maarifa tu ya kupata na kuvuna maji kwa ajili ya kuendeleza kilimo chetu, hatuwezi kuendelea kwa kutegemea mtama, mahindi, zabibu au alizeti pekee lazima tuongeze na mazao mengine” alisema Mhe. Dkt. Mpango.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana amemshukuru Mhe. Dkt. Mpango kwa kukubali TARI kuweka jaribio  la viazi mviringo katika shamba lake  lililopo katika Kijiji cha Mayamaya na kueleza kuwa  kwa sasa TARI imepanga kuweka majaribio ya zao hilo kwa wakulima wadogo wanaolima kwa kutegemea mvua.

Katika hatua nyingine Dkt. Bwane ameongeza kuwa  TARI itaendelea na majaribio ya utafiti wa mazao katika maeneo mbalimbali nchini  ili kuondoa dhana iliyojengeka ya  ikolojia  hii ni ya mazao Fulani pekee na kuwaomba wananchi hususan wakulima  kuwakaribisha TARI kuweka majaribio ya utafiti katika mashamba yao.

Kwa mujibu wa Mtafiti Kiongozi  wa zao la viazi mviringo kutoka kituo cha TARI - Uyole Dkt. Owekisha Kwigizila, mbegu hiyo  mpya ya TARI ina sifa ya kukomaa kwa muda mfupi wa takribani siku 90, kustahimili ukame na baadhi ya magonjwa pamoja na kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 35 hadi 40 kwa hekta moja.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mayamaya walioshiriki katika zoezi la uvunaji wa viazi hivyo wameonesha kustaajabishwa na kustawi kwa zao hilo katika Kijiji hicho cha Mayamaya na kueleza kuwa hiyo ni mara yao ya kwanza kuona zao hilo la viazi likilimwa  na kustawi Mkoani Dodoma na kuonyesha shauku kubwa ya kujaribu kulima zao hilo katika mashamba yao,

Utafiti huo wa zao la viazi Mkoani Dodoma bado unaendelea ili kukamilisha hatua zote muhimu kabla ya mbegu hiyo kuingizwa rasmi sokoni. Mafanikio hayo yanaendelea kuthibitisha kuwa Dodoma inaweza kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kupitia nguvu ya utafiti, ubunifu na teknolojia za kilimo  na kubadilisha maisha ya wakulima wa Mkoa wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment