July 24, 2026

TNCM YAIDHINISHA OMBI LA TANZANIA LA UFADHILI WA MZUNGUKO WA NANE (GC8) WA MFUKO WA DUNIA KWA KIPINDI CHA 2027–2029








Na. Mwandishi wetu - Dar es Salaam
Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu na Kusimamia Fedha za Mfuko wa Dunia nchini Tanzania (Tanzania National Coordinating Mechanism – TNCM), imeidhinisha rasmi Ombi la Tanzania la Ufadhili wa Mzunguko wa Nane wa Mfuko wa Dunia (Global Fund Grant Cycle 8 – GC8) kiasi cha dola za Marekani milioni 538.6 kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu (TB) na Malaria, pamoja na kuimarisha Mifumo Thabiti na Endelevu ya Afya (RSSH), katika kipindi cha utekelezaji kuanzia Januari 2027 hadi Desemba 2029.

Uidhinishaji huo umefanyika jijini Dar es Salaam katika kikao maalum cha TNCM kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNCM.

Dkt. Yonazi amesema kuwa, mchakato wa maandalizi ya Ombi la GC8 ulianza rasmi tarehe 13 Machi, 2026 na umeendelea kwa zaidi ya miezi minne, ukihusisha mashauriano ya kina, majadiliano ya kitaifa, upangaji wa vipaumbele, uandishi wa andiko, mapitio ya kitaalamu na uhakiki wa nyaraka za maombi. 

Aidha, alifafanua kuwa, mchakato huu umejengwa katika msingi wa ushirikishwaji mpana wa wadau, uwazi, uwajibikaji na umiliki wa kitaifa ambapo zaidi ya wadau 270 walishiriki kwa uwakilishi wa makundi mbalimbali, yakiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara, Idara na Taasisi zake; Washirika wa Maendeleo, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Mashirika ya Dini, watu wanaoishi na VVU, jamii zilizo katika hatari kubwa ya maambukizi na zilizoathiriwa na magonjwa hayo; pamoja na wataalamu wa sekta ya afya.

Dkt. Yonazi ameeleza kuwa uwekezaji wa Mfuko wa Dunia umeendelea kutoa mchango mkubwa katika juhudi za Serikali za kuboresha afya na ustawi wa Watanzania, na kusema utekelezaji wa GC8 utatoa fursa kwa Nchi kuendela kuzuia maambukizi mapya ya VVU, kuongeza upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV), kuimarisha kinga, uchunguzi na matibabu ya Malaria, pamoja na kuboresha ugunduzi wa mapema na matibabu ya Kifua Kikuu.

“Kuidhinishwa kwa Ombi hili la Ufadhili ni matokeo ya kazi kubwa na ushirikiano wa wadau wetu ambao wamewekeza muda, utaalamu na rasilimali kuhakikisha kuwa vipaumbele vilivyoainishwa vinazingatia mahitaji ya nchi pamoja na sauti za jamii na makundi yanayoathiriwa na magonjwa hayo”.Alisema Dkt. Yonazi.

Aliongezea kuwa,hatua hiyo ni mafanikio muhimu yanayoonesha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa hayo matatu, sambamba na kujenga mfumo wa afya ulio imara, jumuishi na endelevu.

Dkt. Yonazi ameshukuru Sekretarieti ya Mfuko wa Dunia iliyopo Geneva (Global Fund Country Team), wajumbe wa TNCM pamoja na wadau wote walioshiriki katika maandalizi na ukamilishaji wa maombi hayo, amepongeza jitihada zao akisema zimekuwa na mchango muhimu kuwezesha kufikia hatua hii.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNCM, Bw. Kent Pius, ametoa shukrani maalum kwa Mwenyekiti wa TNCM, Mfuko wa Dunia, wajumbe na wadau wote kwa ushirikiano na uwajibikaji mkubwa katika kuhakikisha kuwa zoezi hili limefanyika kwa ufanisi na ubora uliokusudiwa na kusema kuwa, hatua hii ni matokeo ya dhamira ya dhati na juhudi za pamoja. 

“TNCM itaendelea kuratibu ushirikiano kati ya Serikali, jamii, Asasi za Kiraia, Washirika wa Maendeleo, Sekta Binafsi na wadau wa kimataifa katika kuhakikisha uwekezaji wa Mfuko wa Dunia unachangia katika kufikia malengo ya Kitaifa na Kimataifa ya kutokomeza UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kama vitisho vya afya ya jamii,” alisema Kent.

No comments:

Post a Comment