July 25, 2026

MAWAZIRI WA AFRIKA WAKUBALIANA KUHARAKISHA MAGEUZI YA KIUCHUMI, VIWANDA NA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA





Abidjan, Côte d’Ivoire
Nchi za Afrika zimekubaliana kuweka kipaumbele katika ufadhili wa viwanda vinavyotegemea rasilimali za ndani, hususan madini, pamoja na kuharakisha uongezaji thamani wa bidhaa na kuimarisha biashara ya ndani ya bara ili kujenga uchumi jumuishi, endelevu na wenye ushindani.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayosimamia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini uliofanyika jijini Abidjan, nchini Côte d’Ivoire.

Akizungumza baada ya kuhitimishwa kwa mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alisema nchi wanachama zimekubaliana kuongeza uwekezaji katika viwanda vinavyoongeza thamani ya rasilimali za Afrika, kuimarisha biashara ya kikanda na kupunguza utegemezi wa misaada na ufadhili kutoka nje ya bara na kusisitiza Afrika inapaswa kutumia ipasavyo utajiri wake wa rasilimali pamoja na nguvu kazi ya vijana kwa kuwekeza katika elimu, ujuzi na teknolojia za kisasa ili kuchochea maendeleo ya viwanda, huku ikiondoa vikwazo vya biashara na kuimarisha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

*Kiruswa: Afrika iongeze thamani ya madini yake*

Akichangia mjadala katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana katika kutekeleza mikakati ya uongezaji thamani wa madini ndani ya bara badala ya kuendelea kuuza malighafi.

Alisema Afrika imejaaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini, yakiwemo madini mkakati (Strategic Minerals) na madini muhimu (Critical Minerals) yanayohitajika duniani kwa ajili ya maendeleo ya teknolojia za kisasa, uzalishaji wa nishati safi na maendeleo ya viwanda.

“Ni wakati wa Afrika kunufaika kikamilifu na rasilimali zake kwa kuwekeza katika uchakataji na uongezaji thamani wa madini ndani ya bara. Ushirikiano wa nchi zetu utasaidia kuongeza ajira, mapato, uhamishaji wa teknolojia na kuifanya Afrika kuwa kitovu cha maendeleo ya viwanda vinavyotokana na madini,” alisema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, alisema ili kuharakisha mageuzi ya kiuchumi Afrika ni muhimu kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuboresha miundombinu ya kimkakati na kuondoa vikwazo vya biashara ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Mkutano huo wa siku mbili uliokuwa na kaulimbiu “Financing Africa’s Industrialization for Sustainable Development” ulilenga kuweka mikakati ya kuharakisha maendeleo ya viwanda vinavyotegemea rasilimali za Afrika, hususan madini, na kuimarisha biashara na ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

No comments:

Post a Comment