Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na washiriki wa Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP), unaofanyika katika Ukumbi wa Blue Sapphire, jijini Dar es Salaam, leo tarehe 4 hadi 6 Mei, 2026.
***************
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni sharti la mafanikio katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa unaozidi kubadilika na kuvuka mipaka.Amesema kuwa katika dunia ya sasa, aina nyingi za uhalifu hupangwa, hufadhiliwa na kuratibiwa kwa njia za kidijitali, hali inayohitaji mifumo imara ya kiteknolojia pamoja na ushirikiano wa pamoja ili kuudhibiti kwa ufanisi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Mei 4, 2026, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP), unaofanyika katika Ukumbi wa Blue Sapphire, jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 4 hadi 6 Mei, 2026, wenye kaulimbiu isemayo “Matumizi ya Teknolojia katika Kukabiliana na Uhalifu Dhidi ya Wanyamapori na Uhalifu wa Kimataifa Uliopangwa.”
“Kama ambavyo uhalifu uliopangwa hauwezi kuwepo bila kuvuka mipaka, vivyo hivyo vyombo vya dola na mifumo ya haki ya jinai haviwezi kukabiliana nao kwa ufanisi bila kuwa na mifumo madhubuti ya ushirikiano wa kimataifa, hususan katika maeneo ya msaada wa kisheria na urejeshaji wa watuhumiwa,” alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu mwelekeo wa uhalifu wa kisasa, Waziri Mkuu alisema:
“Utafiti unaonesha kuwa katika hali nyingi, uhalifu dhidi ya wanyamapori na uhalifu wa kimataifa hupangwa kidijitali, hufadhiliwa kwa njia za kielektroniki na kuratibiwa kuvuka mipaka, na pia hufichwa kwa kutumia mbinu tata za kiteknolojia, hali inayofanya mipango na athari zake kuvuka mipaka kwa kasi kubwa ambayo wakati mwingine hupita bila kugundulika.”
Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ni sehemu muhimu ya mafanikio katika mapambano hayo.
“Katika mazingira haya, hatuwezi kufanikiwa katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa uliopangwa bila kutumia kikamilifu teknolojia kama nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto hii ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla,” alisema.
Akizungumzia athari za uhalifu huo, Waziri Mkuu alisema ni tishio kwa uchumi na usalama wa mataifa.
“Ni dhahiri kwamba biashara haramu ya wanyamapori na aina nyingine za uhalifu wa kimataifa uliopangwa ni tishio kubwa kwa mataifa yetu; unachangia kupotea kwa rasilimali zetu na pia ni tishio kwa utulivu na usalama wa nchi zetu,” alisema.
Akielezea hatua zilizochukuliwa na Tanzania, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kuboresha mifumo ya kisheria ili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipitia na kuboresha sheria zake za msaada wa kisheria ili kupanua wigo wa ushirikiano, ikiwemo matumizi ya ushahidi wa kidijitali, ufuatiliaji wa mawasiliano na mbinu za kisasa za uchunguzi,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeondoa baadhi ya taratibu za urasimu ili kuwezesha utekelezaji wa haraka wa maombi ya msaada wa kisheria kupitia mamlaka husika.
Waziri Mkuu alizitaka nchi wanachama kutumia jukwaa la EAAP kama chombo cha kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kubadilishana taarifa.
“Katika dunia ya sasa ambapo uhalifu hauna mipaka, majibu yetu lazima yawe ya pamoja, ya kimkakati na yenye mshikamano,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainabu Katimba, alisema uwepo wa Waziri Mkuu katika mkutano huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika mapambano dhidi ya uhalifu.
Alisema kaulimbiu ya mkutano huo ni ya wakati muafaka na inaakisi changamoto za sasa, akiwahimiza washiriki kutumia jukwaa hilo kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya haki katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Naye Rais wa Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP), ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashtaka wa Jamhuri ya Kenya, Renson Ingonga, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na uhalifu unaobadilika kwa kasi.
Alisema mkutano huo ni fursa ya kujenga mitandao imara ya kitaaluma, kuimarisha uaminifu na kukuza mifumo ya ushirikiano itakayowezesha kukabiliana ipasavyo na uhalifu wa kimataifa uliopangwa.
Mkutano huo wa kimataifa unawakutanisha Wakurugenzi wa Mashtaka, Mawakili Wakuu wa Serikali, viongozi wa vyombo vya sheria pamoja na wadau kutoka mashirika ya kikanda na kimataifa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na mifumo ya haki jinai katika kukabiliana na uhalifu wa kuvuka mipaka.
Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP) kinaundwa na nchi wanachama ambazo ni Tanzania, Burundi, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Msumbiji, Rwanda, Seychelles, Sudan Kusini, Somalia, Malawi, Sudan, Zambia na Uganda.
Akihitimisha, Waziri Mkuu aliwataka washiriki kuhakikisha mkutano huo unazaa matokeo yenye tija kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Kwa maneno hayo machache, natangaza rasmi kufunguliwa kwa Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki,” alisema.

No comments:
Post a Comment