May 03, 2026

TANZANIA NA RWANDA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA ZA BIASHARA, UCHUKUZI NA NISHATI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amempokea Ikulu jijini Dar es Salaam Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame, aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja. 

Rais Dkt. Samia na mwenzake, Rais Kagame wamefanya mazungumzo ya ana kwa ana, na baadaye kuongoza mazungumzo rasmi ya uwili yaliyohusisha ujumbe wa nchi zote mbili, na kufuatiwa na mazungumzo na waandishi wa habari. 

Viongozi hao wamejadili hatua za kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji, uchukuzi na miundombinu, nishati, ulinzi na usalama, uhamiaji, pamoja na uratibu wa misimamo ya nchi hizo mbili katika masuala ya kikanda na kimataifa. 

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania na Rwanda zimeendelea kujenga uhusiano wa undugu, ujirani mwema na urafiki wa kihistoria, unaoakisi mshikamano wa muda mrefu kati ya wananchi wa pande zote mbili. Rais Dkt. Samia amesema biashara kati ya Tanzania na Rwanda imeendelea kukua na kufikia thamani ya shilingi bilioni 644 mwaka 2025. 

Amesema kuanzia mwaka 1990 hadi mwezi Machi, 2026, Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania imesajili miradi 42 ya uwekezaji kutoka Rwanda yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.5, iliyozalisha ajira 2,225 kwa Watanzania. 

Pamoja na hatua hiyo, Rais Dkt. Samia amesema nchi zote mbili zimekubaliana kuongeza kasi ya kuondoa changamoto za kibiashara, ikiwemo vikwazo visivyo vya kikodi, ili kupanua biashara na uwekezaji, na kutumia kikamilifu fursa za soko la pamoja la Afrika Mashariki na Soko Huru la Biashara la Afrika.

Katika uchukuzi na miundombinu, Rais Dkt. Samia amesema takribani asilimia 70 ya shehena za Rwanda hupitia bandari za Tanzania, na kwamba Tanzania itaendelea kuweka mazingira bora ya kuhudumia shehena hizo, ikiwemo huduma maalum katika bandari, matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Tanga, pamoja na maeneo ya kuhifadhi mizigo. 

Marais hao pia wamejadili uendelezaji wa miundombinu ya reli na barabara, ikiwemo mradi wa reli ya Isaka hadi Kigali, unaolenga kuharakisha usafirishaji wa bidhaa na kuongeza ufanisi wa biashara kati ya nchi hizo mbili. 

Katika nishati, viongozi hao wamejadili Mradi wa Umeme wa Maporomoko ya Rusumo, unaozihusisha Tanzania, Rwanda na Burundi, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 80, pamoja na makubaliano ya kuuziana umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme la Rwanda (REG), kwa ajili ya kuchochea shughuli za kiuchumi kwa manufaa ya nchi zote mbili. 

Kwa upande wake, Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Dkt. Samia na Watanzania kwa mapokezi mazuri, akisema Tanzania ni mshirika muhimu wa Rwanda, hususan katika biashara na usafirishaji kupitia bandari zake zinazoiunganisha Rwanda na masoko ya kimataifa. 

Rais Kagame amesema Tanzania na Rwanda zinapaswa kuimarisha msingi imara wa uhusiano uliopo kwa kuendeleza ushirikiano katika maeneo ya kimkakati ili kukuza biashara, kuendeleza miradi ya pamoja na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya nchi hizo mbili. 

Aidha, amesema Rwanda itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania katika kuimarisha ushirikiano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika na majukwaa mengine ya kimataifa, kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili. 

Ziara ya Rais Kagame nchini inadhihirisha nafasi muhimu ya Tanzania katika biashara na ushirikiano wa kikanda, kama mshirika wa karibu na lango la biashara kwa nchi jirani, huku makubaliano yaliyofikiwa yakitarajiwa kuongeza biashara, kurahisisha usafirishaji na kufungua fursa zaidi kwa wananchi wa nchi zote mbili.

No comments:

Post a Comment