Mkurugenzi wa Milki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Upendo Matotola, ameibuka mshindi miongoni mwa washindi wa Tuzo ya WIMA (Women in Management Africa) kwa mwaka 2026, kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza na kuimarisha sekta ya milki nchini.
Tuzo hiyo ni ushahidi wa uongozi wake mahiri, unaodhihirishwa na kujitolea kwake kuimarisha utendaji wa sekta ya milki pamoja na kuleta mabadiliko chanya yenye tija kwa jamii.
Mafanikio haya yanaakisi si tu ubora wake kitaaluma, bali pia mchango wake katika kusukuma mbele maono ya Afrika yenye ushirikishwaji mpana na maendeleo endelevu.
Dkt. Upendo alikabidhiwa tuzo hiyo mwishoni mwa wiki katika hafla maalum ya kuwapongeza na kuwatunza wanawake viongozi waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za uongozi barani Afrika. Hafla hiyo iliendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo, “Alama, uongozi na matokeo endelevu.”
Women in Management Africa (WIMA)ni taasisi ya bara la Afrika inayojikita katika kutambua, kusherehekea na kukuza wanawake viongozi bora wanaochangia mabadiliko ya sekta mbalimbali, kuboresha maisha ya jamii, na kuendeleza ukuaji wa Afrika katika ngazi ya kimataifa.



No comments:
Post a Comment